November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC akoshwa na elimu ya saikolojia

Na Esther Macha , Timesmajira Online,Mbeya

KAMANDA wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ,Benjamin Kuzaga anatarajia kutembelea shule ya msingi na awali ya Holyland Novemba 2 mwaka huu iliopo Chunya mkoani hapa.

Hatua hiyo ya Kamanda Kuzaga kufanya ziara hiyo katika shule hiyo ni kufuatia uwepo wa taarifa za kuwa shuleni hapo wanatumia wenye taaluma ya saikolojia kuzungumza na wanafunzi ambao wamekumbana na changamoto mbalimbali pamoja na kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia.

Kamanda Kuzaga ambaye yuko katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kata kwa Kata ,kuzungumza na wanafunzi shuleni,kanisani,misikitini ,vyuoni pamoja na kutoa elimu ya kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Mbali na kuzungumza na wanafunzi pia atazungumza na walimu wa shule hiyo lengo ni kuhakikisha wanaongeza ubunifu zaidi katika kuboresha sekta ya elimu.

“Ubunifu walioonesha walimu hawa unapaswa kuigwa na shule zingine ili kuweza kuwaweka sawa watoto kimasomo,”amesema.

Lawena Nsonda (Baba mzazi) ni Mkurugenzi wa shule hiyo amesema kuwa walimu wa somo la Saikolojia ni msaada mkubwa sana kwa watoto hasa wale wanaonekana kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoelewa wakati wa kufundisha masomo darasani.

“Tuna mwalimu ambaye ni maalum kwa ajili ya kusaidia watoto wetu ambao tumeona matunda makubwa juu ya ufundishaji wa somo hili na limekuwa msaada sana kwani tayari tulikuwa na watoto wenye changamoto hizo walimu wamefanya kazi na sasa wapo vizuri darasani, “amesema Mkurugenzi huyo.

Jana mtandao wa Timesmajira ulitoa taarifa ya shule ya mchepuo wa kiingereza ya Holyland iliyopo katika Mji mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya kufundisha somo la Saikolojia kwa wanafunzi ambao wanaonekana kuwa changamoto ya kutoelewa darasani na muda mwingi kukosa raha kipindi cha masomo.

Timesmajira ilifika katika shule ya Holyland iliyopo katika Mji mdogo wa Makongolosi wilaya ya Chunya October 27 mwaka kuona utoaji wa elimu katika shule hiyo ambayo kwa Makongolosi ndo shule pekee ya mchepuo wa kiingereza.