Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline
BAADA ya zaidi ya miaka 66 ya ushirikiano wa kihistoria, hatua mpya inaanza katika tasnia ya habari
Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) imetangaza kuuza hisa zake zote katika kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited, inayomiliki asilimia 54.08 ya hisa za Nation Media Group (NMG), kwa kampuni ya Taarifa Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Afrika Mashariki Rostam Azizi.
Uamuzi huu unahitimisha safari iliyoanza mwaka 1959, wakati vyombo vya habari vya Nation vilipoanzishwa kwa lengo la kujenga vyombo vya habari huru na vinavyoaminika Afrika Mashariki. Kilichoanza kama gazeti la Kiswahili Taifa Leo, leo kimekua kuwa kundi kubwa la vyombo vya habari lenye zaidi ya brand 30, likifikia zaidi ya watumiaji milioni 62 wa kidijitali katika nchi kadhaa za ukanda huu.
Katika historia yake, NMG imekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya demokrasia na utoaji wa taarifa sahihi kwa jamii. Kuanzia uzinduzi wa Daily Nation mwaka 1960, kuorodheshwa kwenye soko la hisa la Nairobi mwaka 1973, hadi kuongoza mageuzi ya habari za kidijitali barani Afrika.
Kupitia uwekezaji mpya wa Taarifa Ltd, NMG inatarajiwa kuimarisha zaidi mageuzi ya kidijitali, kuongeza ubunifu wa habari na kuendelea kuhudumia wasomaji kwa uandishi wa habari wenye maslahi ya umma.
Wakati huo huo, taasisi za mtandao wa Aga Khan zitaendelea kuendeleza taaluma ya uandishi wa habari kupitia Aga Khan University – Graduate School of Media and Communications, inayofundisha kizazi kipya cha wanahabari barani Afrika.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 3–4 ijayo, baada ya kupata idhini zote za kisheria.

More Stories
Wizara ya nishati yapokea Tril.1.15 za miradi ya Maendeleo
REA yapongezwa kuwawezesha wandelezaji wadogo wa miradi Umeme
Serikali kuendelea kupeleka huduma kwa Wananchi