Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Kigoma
Mwanahabari na msomi mashuhuri Rose Mweko ametangaza rasmi azma yake ya kuwania ubunge kupitia kiti maalum cha wanawake kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akilenga kuwakilisha Mkoa wa Kigoma katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hilo limethibitishwa baada ya Mweko kukabidhi fomu ya kugombea katika ofisi za CCM Mkoa wa Kigoma, hatua inayoweka wazi dhamira yake ya kuingia katika ulingo wa kisiasa kwa mara ya kwanza.
Mweko amejizolea heshima katika tasnia ya habari kupitia kazi yake ndani ya mtandao wa Uhuru Publications Limited, chombo cha habari kinachomilikiwa na CCM. Kupitia nafasi hiyo, amekuwa mstari wa mbele kuibua na kuangazia masuala yanayohusu maendeleo ya jamii, haki za wanawake, elimu, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kukabidhi fomu, Mweko, amesema,”Niminaingia katika siasa si kwa sababu ya kutafuta mamlaka, bali kwa sababu ya kuitikia wito wa wananchi hasa wanawake na vijana wa Kigoma, wanaotaka kiongozi anayewasikiliza, anayewawakilisha kwa sauti ya kweli, na mwenye maono ya maendeleo jumuishi,”.
Mweko ameahidi kuwa, endapo atapata nafasi hiyo, atajielekeza zaidi katika kuinua elimu kwa watoto wa kike, kuwezesha wanawake kiuchumi, na kushiriki kikamilifu katika kutunga sera zenye tija kwa ustawi wa jamii ya Kigoma.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi