November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RMO: Wachimbaji wanufaike, haki za mwenye leseni zilindwe

Na Mary Margwe, TimesMajira Online

Kampuni ya Franone Mining inayochimba Madini ya Tanzanite Kitalu ‘ C ‘ katika Mjini Mdogo wa Mirerani iko kwenye mgogoro wa mitobozano ya mipaka ya chini na wachimbaji wadogo wakidai kuwa mipaka ya leseni iko juu, jambo ambalo Serikali imefafanua kuwa mipaka ya leseni iko mpaka chini.

Aidha itambulike kuwa kwenye Mgodi wa Kitalu ‘ C ‘ Serikali ina miliki hisa asilimia 16, wakati Kampuni ya Franone Mining nayo ikimiliki asilimia 84, tangu wapatiwe leseni.

Awali katika ziara ya Waziri wa Madini Mh.Antony Peter Mavunde mwezi mmoja uliopita akiwa Mirerani, pamoja na mambo mengine aliweza kukaa kikao na baadhi ya wamiliki wa migodi, na wachimbaji na wafanyabiasharawa Madini ya Tanzanite katika ukumbi wa Songambele aliweza kutoa ufafanuazi juu ya namna leseni ya uchimbaji inavyomilikiwa.

Hii inakuja kufuatia baadhi ya wamiliki wa migodi wakidai kuwa Kampuni ya Franone imeingia mitobozano ya mipaka ya chini na wachimbaji wadogo wanaodai kuwa Mipaka ya leseni chini hakuna mipaka, jambo ambalo Waziri wa Madini Antony Mavunde ametoa ufafanuzi wa Kisheria kuwa mipaka ya leseni inaenda mpaka chini.

Afisa Madini Mkazi Mirerani ( RMO ) Chacha Marwa Nchagwa hapa anatoa ufafanuazi juu ya mgogoro huo akiwa kwenye mkutano wa mwisho wa Mwaka wa Wachimbaji Madini ya Tanzanite ulifanyika katika ukumbi wa Songambele Mji Mdogo wa Mirerani chini ya Mwenyekiti wa Wachimbaji Tawi la Mirerani Jumanne Athuman Nahe, na Katibu wake Rachel Njau.

Nchagwa anasema ” Kama tunavyofahamu Nchi inaongozwa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu, wale ambao walikuwepo kwenye kile kikao ambacho Waziri wa Madini Mh.Antony Peter Mavunde alikuwepo kwenye ukumbi huu tulipata ujumbe wa moja kwa moja kwamba Mipaka ya leseni inaenda mpaka chini, kinyume na ambavyo Mirerani tumekuwa tukisema chini hakuna mipaka, lakini tulipata ufafanuzi wa Kisheria na tukaelezwa hivyo” anasema Nchagwa.

SERIKALI IKISHAMPATIA MTU LESENI NINI KINAFANYIKA

” Serikali sisi tukishampatia mtu Leseni tunampa hati ya kutafiti na kuchimba kwenye eneo lake, na hati hiyo anakua nayo kama vile mtua anayepewa hati yake kumiliki eneo lake la kiwanja anavyopewa na ardhi kwahiyo yeye anapaswa apange mpango au utaratibu wa kuendesha shughuli za uchimbaji katika eneo lake” anasema Nchagwa.

Aidha anasema hilo ni tamko la Kisheria anatakiwa aandae Manual Planning kwa kila mwenye leseni hususani hizo zenye leseni kubwa ” Tunakumbuka kuwa ambao walikua wakifamya shughuli zao siku za nyuma kabla ya kumpatia Mwekezaji eneo hilo, tulichokifanya sisi tuliitana wote tunafanya kazi Moja na tunafahamiana shughuli zetu zinavyokwenda na tukaambiana.

Nchagwa anafafanua kuwa ” Wajibu wa kutoa idhini ya kuchimba ndani ya leseni ya mtu anayo mwenye leseni mwenyewe, sisi kama serikali hatuwezi tukaamua tukamuamrisha kwamba ni lazima hawa watu wachimbe ndani ya leseni ya yako, hilo halipo kabisa, wote tupo hapa tunaomiliki leseni, chukulia leo hii mimi naamka RMO nakuja kwenye leseni yako nasema bwana nimekuletea mtu hapa ana shimo lake lazima muendelee kuwa kwahiyo tunaacha hilo hasa kwa wamiliki wa leseni ” anasema RMO Nchagwa.

Aidha anasema kama vile anasisitiziwa kwamba hawa wameingia gharama kwenye eneo lako tulichokifanya tumewaambia kaeni sasa mzungumze jambo ambalo linaruhisiwa na Serikali inalitambua pale ambapo Mwenye leseni anakua anakubaliana na mwingine ambaye anafanya kazi ndani ya leseni yake.

” Tunafahamu Tanzania wamiliki wa leseni wamekuwa ni Wachache, lakini wachimbaji wanaofanya kazi kwenye leseni hizo wanakuwaga ni wengi au wale wanaokuwa na mashimo ndani ya leseni unaweza ukawa na leseni lakini leseni hiyo ikawa na mashimo mengi ambayoyana milikiwa na Watu tofauti tofauti, sio sheria lakini ni utaratibu ambao unafanyika na wanakua wanakubaliana.

Aidha Nchagwa anafafanua wamekubaliana kwahiyo wakaona wakae na kukubaliana sasa ni namna gani mnaendesha shughuli zenu ndani ya eneo la Kitalu ‘C’, wakakae wakakubaliana lakini mwelekeo ulikua sio kuwatoa kwamba tokeni hapana watafute mahali unarudi nyuma wawe wanachimba huku mnaelekea kurudi kwenye eneo lenu.

” Na ndio ilikua hivyo hususani wale waliotokea Kitalu B mwenye leseni alisema kadili watakavyokutana wataendelea kuelewana, hasa hata mwenye leseni hajalalamika kwa Serikali, sisi hatuwezi kwenda kuwaambia watu wa Kitalu B kwamba jamani eeeh ondokeni lakini pale itakapotokea kuna mwingiliano wa utendaji kazi tutakaa tutashirikiana na Kamati zetu tutasuruhisha” anasema Nchagwa.

Aidha anafafanua kuwa lengo likiwa ni kwamba kila mchimbaji aliyemwaga jasho lake kwenye eneo husika aweze kunufaika, lakini pia haki za mwenye leseni ziweze kulindwa na Serikali ili mwisho wa siku tutakapomuuliza kwamba kwanini hujafanya hili na lile asije akasema ni kwasababu mlinilazimisha nifanye kazi na mtu fulani tumeelewana” amefafanua Nchagwa.

Kwahiyo suala la Kitalu ‘C’ bado tunaendelea kulifanyia kazi Kwa kutumia sheria, lakini pia kutumia busara na mahusiano ambayo tunaendelea kuwa nayo kwenye eneo la Mirerani, wengi tuliopo hapa tunafahamiana hakuna mgeni aliyetokea nje ya Mirerani kwahiyo tunazungumzia Kwa lugha ambazo tunaelewana na tunaendelea kuifanyia kazi.

USHAURI WA MAREMA JUU YA KITALU ‘C ‘ NA WACHIMBAJI WADOGO

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha wachimbaji Mkoa wa Manyara ( MAREMA ) Tawi la Mirerani Rachel Njau anasema Chama Cha wachimbaji Tawi la Mirerani limetoa Mapendekezo kuwa lengo kuu ni kuhakikisha Mwekezaji na mchimbaji mdogo pande zote mbili ziweze kuwa salama bila kuasili upande mmoja.

Njau anasema pia Chama kimependekeza kuwe na rasimu itakayotumika kutatua Migogoro midogo na kamati za usuruhishi migodini ipewe meno ili iweze kusuluhisha pia mitobozano au changamoto za wachimbaji wakubwa, hii itasaidia katika kuondokana na Migogoro iliyoko ndani ya ukuta wa Magufuli.

” Tulikua na changamoto mbalimbali kama mlivyosikia katika mkutano wetu wa mwisho mwa mwaka kuwa wachimbaji wadogo wa mpakani wana changamoto na Mwekezaji lakini kama Chama tumeomba tupewe au tumuombe RMO na Mwekezaji aliyepo na wale wenye changamoto nao tukae tuzungumze, kwasababu masuala ya mpakani hayajaanza leo ni changamoto ya muda mrefu, na safari hii Mwekezaji aliyekuwepo ni Mtanzania na alikua mchimbaji mdogo na nina uhakika ni msikivu na mzalendo, tuweze kujua Nini tunaweza kufanya ili tuweze kuwa salama pande zote mbili bila kuasili upande mmoja” anasema Rachel Njau.

Hata hivyo Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani Jumanne Athuman Nahe anasema RMO Nchagwa amealikwa Mgeni rasmi katika mkutano huo na amefafanua vizuri juu ya Kitalu C na wachimbaji wadogo Kwa lengo la kupata muafaka wa jumla.

Nahe anaongeza anaimba serikali na Bunge kuhakikisha inabadilisha Sheria ya Vertical hasa hasa kwa eneo la Mirerani kwasababu Tanzanite inachimbwa kutokana na ulalo wa Mwamba unakoelekea.

” Sasa sisi kama wadau na viongozi wa vyama vya Wachimbaji tunaiomba Serikali ishirikiane na wadau na wachimbaji katika kuhakikisha inasikiliza kero za wachimbaji Kwa kutoa muafaka bila kuumiza upande mwingine” anaongeza Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani Nahe.