September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ripoti ya SBL yatekeleza miradi zaidi ya 20 nchini

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Serengeti Breweries (SBL) imeendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza miradi zaidi ya ishirini nchini inayoonyesha mafanikio mengi katika nyanja ya Elimu, Maji, Mazingira hususani kwenye maendeleo na ukuaji wa uchumi.

SBL imeendelea kujikita katika kuzisaidia jamii kupata uhakika wa maji safi, kwa kutimiza hilo imefanikiwa kutekeleza miradi zaidi ya ishirini nchini, ukiwemo mradi wake wa tanki kubwa la kutibu maji lililopo kata ya Basuto, Mkoani Manyara

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya shughuli endelevu chini ya kampuni tanzu ya East Africa Breweries Limited (EABL) Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa SBL John Wanyancha amesema mradi wa maji kata ya Basuto umesaidia zaidi ya watu elfu 14 na kuzalisha lita laki tisa za maji ndani ya masaa 12, zaidi ya hitaji la maji katika eneo hilo.

“SBL inajivunia kuwa mstari wa mbele katika kuchochea maendeleo endelevu kwa njia ya ubunifu na ya kipekee inayoakisi ujumuishi, tunategemea kuendeleza mpango huu kwa kutimiza malengo mengi” Amesema Wanyancha

Aidha, Katika kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu matumizi ya pombe, SBL inatumia kampeni yake ya unywaji kistarabu, endesha kistarabu, Jifunza kuhusu pombe kupitia tovuti maalum ya DrinkiQ na imewafikia zaidi ya madereva 5000, wanafunzi 8,200 juu ya unywaji katika umri mdogo na kuwashawishi zaidi ya watu 2000 kujifunza kuhusu matumizi ya pombe ndani ya mwaka 2022.

Hivyo, SBL ilitoa ufadhili wa masomo ya kilimo kupitia programu yake ya Kilimo Viwanda,iliyofadhili zaidi ya wanafunzi 200 wanaotoka katika familia zisizo na uwezo huku wanawake na watu wenye ulemavu na kupanda miti zaidi ya 5,000 wilayani Kongwa, mkoani Dodoma.

Naye Meneja Kanda ya Mashariki kutoka NEMC Hamadi Taimur Kissiwa, amesema kuwa SBL inaonyesha kwa mfano ilivyo muhimu kwa wawekezaji na makampuni kufanya kazi zao kwa kuzingatia mazingira na masuala ya tabia nchi.

“Karibu asilimia mia moja ya plastiki zote katika viwanda vyetu chakatwa na kutumiwa upya na kuozeshwa. Hii ni ongezeko la juu zaidi ya mwaka 2022 ambapo asilimia tisini ya plastiki zetu zilichakatwa tena na zaidi ya 2022 ambapo tuliweka lengo la asilimia tisini na nane”

Kwa upande wake Kaimu mkuu wa chuo cha Kaole Wazazi College Maxmillian Sarakikya amesema mchango wa SBL kwenye elimu ni muhimu “ Hii kampuni imefanya jambo kubwa sana kuinua vijana kimasomo hasa kilimo, tendo la kuigiwa kama mfano na makampuni na wadau wengine wa elimu.

Mwakilishi kutoka FDH Michael Salali, ambaye ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo inayoshirikiana kwa ukaribu na SBL aliongeza kwa kusema “Tunajivunia kushirikiana na SBL katika agenda ya kutanua ujumuishi na utofauti wa watu, katika hilo SBL imewainua watu wenye ulemavu kwa kuwapa mafunzo ya kilimo, fedha na ujuzi”