December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ripoti: Wanaume wanaofanya kazi muda mrefu wanafariki kwa wingi

GENEVA, Utafiti uliofanywa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kazi Duniani (ILO) umebainisha ongezeko la asilimia 29 la vifo vitokanavyo na magonjwa yanayosababishwa na kufanya kazi muda mrefu huku wanaume wakitajwa kuwa ndio wahanga wakubwa.

Katika taarifa yao ya pamoja kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Geneva nchini Uswisi, utafiti huo umefanyika katika nchi 154 na matokeo yanaonesha kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa watu wengi zaidi watapoteza maisha hususan kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona ambapo watu wanajikuta wanafanya kazi kwa muda mrefu.

Ceridwen Johnson Afisa kutoka WHO amesema, “saa nyingi za kufanya kazi zimesababisha vifo vya watu 745,000 kutokana na ugojwa wa kiharusi na matatizo ya moyo kwa mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 29 tangu mwaka 2000 kwa mujibu wa makisio yaliyofanywa na shirika la WHO na ILO,”amesema. 

Ripoti ilieleza kuwa, kufanya kazi saa 55 kwa wiki au zaidi kunamuweka mtu katika hatari ya kupata kiharusi na kufa na magonjwa ya moyo ikilinganishwa na kufanya kazi kati ya saa 35 adi 40 kwa wiki.

“Magonjwa yanayosababishwa na ajira yanawakumba sana wanaume, asilimia 72 ya vifo vinatokea kwa wanaume, watu wanaoishi Pasifiki Magharibi na Ukanda wa Kusini Mashariki mwa nchi za Asia, watu wazima na wazee.

“Vifo vingi vilivyorekodiwa vilikuwa watu wenye umri wa miaka 60 mpaka 79 ambao wamefanya kazi kwa saa 55 kwa wiki wakiwa kati ya umri wa miaka 45 na 74,”amesema Johnson.

Hata hivyo, ushauri umetolewa kwa serikali, wafanyakazi na asasi za kusimamia maslahi ya wafanyakazi kuanzisha sheria, sera na kanuni za kuzuia muda mrefu wa ziada kufanya kazi baaada ya saa za kazi za kawaida kuisha.