June 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ripoti: Ukatili dhidi ya watoto nchini umepungua

Na Imma Mbuguni, TimesMajira Online, Dar es Salaam

TANZANIA imeweka historia mpya katika ulinzi wa haki za watoto kwa kuzindua rasmi matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024, yakionesha kupungua kwa viwango vya ukatili wa kingono, kimwili na kihisia nchini kote kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na utafiti wa awali wa mwaka 2009.

Matokeo hayo yametangazwa jana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, huku akiweka msisitizo kuwa utafiti huu unaonesha kuwa juhudi za Serikali na washirika wake zimezaa matunda.

Hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, ikihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania, wawakilishi wa Serikali ya Marekani, wawakilishi wa UNICEF, CDC, NBS, OCGS, THPS na wadau wengine wa maendeleo.

Gwajima amesema “Takwimu zinaonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 15, kwa kushirikiana na familia, jamii, taasisi na vijana wenyewe,”

Utafiti huu ulihusisha vijana zaidi ya 11,000 wenye umri wa miaka 13 hadi 24, kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, na ulifanyika kati ya Machi na Juni 2024.

Aidha Waziri Gwajima alikiri kuwa licha ya mafanikio haya, bado takribani matukio 1,100 ya ukatili dhidi ya watoto huripotiwa kila mwezi nchini, kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi.

Hivyo, alisema juhudi zinaendelea ili kuimarisha zaidi ulinzi wa watoto.

Baadhi ya hatua zinazochukuliwa ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Mtoto ili kuondoa mapungufu, utekelezaji wa MTAKUWWA Awamu ya Pili (2023–2030) pamoja na kampeni ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni ili kulinda watoto dhidi ya hatari za kidijitali.

Hatua zaidi ni pamoja na huduma kwa manusura wa ukatili kupitia vituo 32 vya Mkono kwa Mkono, kuokoa watoto wa mtaani na kuwawezesha kielimu na kijamii pamoja na kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari na maafisa wa serikali kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Marekani, Balozi mdogo wa Marekani(Chargé d’Affaires a.i.), Andrew Lentz, alielezea jinsi Marekani ilivyofurahia kuwa sehemu ya mafanikio haya kupitia ufadhili wa mpango wa PEPFAR na usaidizi wa kiufundi kutoka CDC.

“Kuna siku tutashuhudia kila mtoto wa Tanzania akiwa na stadi za maisha, kinga dhidi ya VVU, msaada wa ustawi wa kijamii, walimu waliopata mafunzo ya kutambua ishara za ukatili, na vituo vya huduma jumuishi katika hospitali za wilaya,” alisema Lentz.

Aliongeza kuwa VACS ni mfano wa sera bora za umma zinazotegemea ushahidi wa kisayansi, na kwamba Tanzania imekuwa kinara duniani tangu kuwa nchi ya kwanza kufanya utafiti wa kitaifa wa aina hii mwaka 2009.

Aidha viongozi wote waliotoa hotuba walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Serikali, asasi za kiraia, familia, na jamii nzima katika kupinga ukatili.

“Tuna ndoto ya Tanzania ambako kila mtoto analelewa kwa upendo, analindwa kwa sheria, na anapewa fursa ya kufikia ndoto zake,” alisema Dkt. Gwajima.

Kwa mujibu wa Waziri, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya sera na sheria zilizopo, ili kuhakikisha zinaboresha huduma kwa manusura na kuzuia ukatili kwa makundi yote ya kijamii.

Wote walikubaliana kuwa ujasiri wa maelfu ya vijana walioshiriki kwenye utafiti huu ni msingi wa mabadiliko. Kauli ya mwisho kutoka kwa wawakilishi wa Marekani ilisomeka:

“Marekani inajivunia kuwa mshirika wa Tanzania katika kujenga mustakabali salama, imara na wenye mafanikio kwa watoto wa nchi hii.”

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto (WMJJWW), Khatib Mwadini Khatib, akimwakilisha Naibu Waziri wa wizara hiyo,  Anna Athanas Paul, alisema kuwa miongoni mwa juhudi zilizotajwa ni utekelezaji wa Sheria ya Watoto namba 6 ya mwaka 2011, Mpango wa Taifa wa Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017-2022), kuanzisha madawati ya Polisi ya Jinsia na Watoto, na kuimarisha vituo vya mkono kwa mkono pamoja na huduma za ustawi wa jamii.

“Mfumo wa elimu umekuwa ukizingatia malezi bora kwa watoto, kuelimisha watoto na wanafunzi katika shule na madrasa ili kujikinga na ukatili, na kuwepo kwa huduma ya simu ya kuwasaidia watoto kuripoti matukio ya ukatili kupitia namba 116,” ameongeza Khatib.