Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline.
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amemkabidhi cheti Cha Pongezi Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly kwa kuthamini mchango wake katika kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia Mkoani Mara.
Dkt. Gwajima amesema kuwa, juhudi zinazofanywa na Rhobi katika kupinga vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni zimeendelea kusaidia wasichana wengi Mkoani Mara kuwa salama, na kuwawezesha kupata elimu ili wafikie ndoto zao kimaisha.
Dkt. Gwajima amemkabidhi cheti hicho Februari 12, 2026 wakati wa Kilele cha kupinga ukeketaji kilichofanyika kitaifa katika Kijiji cha Losirwa Kata ya Esilalei Wilayani Monduli Mkoani Arusha. Kauli mbiu ya kupinga ukeketaji kwa mwaka huu inasema “Sauti yetu tokomeza ukeketaji”.
Katika hotuba yake Waziri Dkt. Gwajima amesema mapambano ya kupinga ukeketaji yanapaswa kufanywa na kila mmoja katika Jamii ili kuhakikisha ustawi bora kwa watu wote unazidi kuimarika. Huku akisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa ukatili kwa ukaribu.

Pia, amewataka Wanaume kusaidia kupata majawabu ya kukomesha ukeketaji katika Jamii sambamba na kuwaendeleza Watoto wa kike kwa kuwapa elimu bora kwa faida ya Jamii na Taifa pia.
Kwa upande wake Rhobi Samwelly akizungumza na Waandishi wa Habari amesema kuwa, anashukuru kuona juhudi anazozifanya zinatambuliwa na kuungwa mkono na serikali.
“Ni faraja kubwa kwangu kupewa cheti hiki, kimenipa nguvu, ari na molari ya juu kuzidisha mapambano ya ukatili. Lengo ni kuona wasichana wanaendelea kuwa salama, kupata elimu, na kutumia fursa mbalimbalikujiletea maendeleo.”amesema Rhobi.
Ameongeza kuwa, ataendelea kushirikiana na wadau pamoja na serikali kuhakikisha juhudi za mapambano ya ukatili zinakiwa endelevu na zinaleta matokeo makubwa katika Jamii na Taifa pia.
Hope for girls and Women in Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni katika kituo Cha ‘Hope Mugumu Nyumba salama’ na kituo Cha ‘Nyumba salama Kiabakari Butiama.
Wakiwa katika vituo hivyo, wasichana hao hupewa elimu, msaada wa kisaikolojia, kuendelezwa kielimu, mafunzo na ujuzi wa fani mbalimbali. Huku kazi nyingine inayofanywa na Shirika hilo ikiwa ni Kutoa elimu ya ukatili wa Kijinsia kwa jamii.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama