Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online
WAKATI msafara wa kikosi wa Simba ukiondoka hapa nchini leo alfajiri (saa 9:45) kuelekea Afrika Kusini kupitia Kenya kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Mei 15 dhidi ya Kaizer Chiefs, wenyeji wao tayari wameshaingiwa baridi kutokana na rekodi bora waliyoiweka Simba katika hatua ya Makundi.
Msimu huu Simba wamekuwa bora huku wakifanikiwa kumaliza hatua hiyo wakiwa kileleni mwa Kundi A baada ya kufikisha alama 13 walizopata baada ya kushinda mechi nne, sare moja na kupoteza mechi yao ya mwisho dhidi ya Al Ahly.
Simba pia walifanikiwa kuweka wavuni goli tisa na kuruhusu goli mbili pekee moja katika ushindi wa goli 4-1 dhidi ya AS Vita na nyingine ni katika mchezo dhidi ya Ahly uliomalizika kwa goli 1-0.
Licha ya rekodi hiyo katika Ligi Mabingwa lakini Simba wameendelea kuwa bora ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) baada ya kushinda mechi tano mfululizo wakiwafunga Mtibwa goli 5-0, Mwadui 1-0, Kagera Sugar 2-0, Gwambina 1-0 na Dodoma Jiji 3-1.
Rekodi hizo ni tofauti na zile za wapinzani wao walioshinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi moja lakini wakifunga goli tano na kuruhusu goli sita huku katika Ligi yao ya ndani wakipoteza mechi tatu dhidi ya Cape Town City, Chippa United na Tshakhuma, wakitoka sare na Bloem Celtic na Baroka FC na kushinda goli 2-1 dhidi ya vinara wa Ligi hiyo, Mamelodi Sundowns.
Tofauti kubwa iliyopo katika rekodi za timu hizo mbili ndio iliyopelekea timu hiyo juzi kucheza mechi ya kirafiki kupima silaha zao dhidi ya timu ya Swallows na kupata ushindi wa goli 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa FNB, haukutangazwa wala kuoneshwa kwenye televisheni lakini pia mashabiki hawakuruhusiwa kuingia uwanjani.
Saidi Yusuph ambaye ni raia wa Tanzania anayeishi nchini umo, amesema kuwa, toka Mei 4 walipocheza dhidi ya Tshakhum na kufungwa goli 2-1 timu hiyo imekuwa ikifanya mazoezi yao kwa kificho wakihofia mbinu zao kunaswa na ‘mashushushu’ wa Simba.
Kuelekea katika mchezo huo, benchi la ufundi la Simba linaloongozwa na Didier Gomes Da Rosa limeweka wazi kuwa, tayari wameshafanyia video za wapinzani wao na wameshaandaa programu maalum ambayo itawaongoza kupata ushindi.
Kocha huyo amesema kuwa, kwa sasa kazi iliyo mbele yao ni kwenda sawa na program yao watakayoendelea kuifanya nchini humo kwani kikosi chao kitaondoka leo jioni ili kwenda kuanza haraka maandalizi na kuzoea hali ya hewa katika mji huo ambapo ni ya ubaridi.
“Baada ya kuahirishwa kwa mchezo wachezaji walilazimika kubaki kikosini kwani tutaondoka Tanzania Jumatatu jioni hivyo ni muhimu kuzingatia katika mchezo wetu ujao wa robo fainali dhidi ya Kaizer Chief,” amesema Gomes.
Kocha huyo alisema kuwa, anafahamu kuwa baada ya kutopata matokeo mazuri katika mechi zao tatu wakipoteza mbili dhidi ya Chippa United na Tshakhuma huku wakitoka sare na Bloem Celtic inayowaweka wapinzani wao kaatika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi watakuwa kwenye presha kubwa ya kutaka matokeo mazuri nyumbani katika michuano hiyo.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025