January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rekodi ya Makonda yawakosha wananchi wa Kakonko Kigoma

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KATIBU wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda, amevunja rekodi kwa kuwa kiongozi bora tangu ateuliwe katika nafasi hiyo kwa kufanya mikutano mingi ya adhara na kutatua kero za wananchi ndani ya mwezi mmoja hali iliyowavutia wanachama na Watanzania.

Hayo yemedhibitishwa na wananchi na viongozi wa Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma, akiwemo Diwani wa Kata ya Kakonko, Augustino Linze wakati wakizungumza na Gazeti la Majira leo, kuhusu ziara ya Mwenezi Makonda mkoani humo.

“Tangu ameteuliwa amevunja rekodi kwa wenezi waliopita, kwa muda mfupi amefanya ziara kwenye mikoa mingi, namna anavyokwenda inawavuta wanachama na watanzania kwa ujumla kwasababu pale anapokuta tatizo analitatua na kulipatia majibu, kama ni ishu ya wakubwa atawapigia simu ili atoe majibu sahihi ili watu wale wabaki na amani”

Aidha Diwani Linze amesema Mwenezi Makonda uongozi wake ni wa tofauti lakini ni uongozi ambao unakwenda kuimarisha na kujenga Chama kwa asilimia kubwa kwani ataongeza nafasi kubwa ya ushindi wa kishindo kikubwa katika chaguzi za serikali ya mitaa mwaka huu.

“Nina Imani kubwa na Katibu wetu mwenezi ndugu Paul Makonda kwa kazi anayoifanya, kwani ataongeza nafasi kubwa ya ushindi kuwa ushindi wa kishindo kikubwa”

“Kakonko kichama tupo vizuri tuna uhakika wa ushindi kuanzia vitongoji, vijiji hadi Madiwani, mpaka sasa hatuna kiti hata kimoja ambacho tulikipoteza mwaka 2020 na tuna uhakika 2024 chaguzi za serikali tutakwenda vizuri na 2025 ushindi kwenye Wilaya yetu ya Kakonko utakua ni wa kishindo” Ameongeza Diwani Linze

Diwani huyo amesema wanaimani na namna Mwenezi Makonda anavyokwenda kwani anauwezo wa kupambana vyama vya upinzani ambapo hadi sasa tangu kuteuliwa kwake nguvu ya vyama vya upinzani imepungua kwa asilimia kubwa.

“Tumepata mwenezi ambaye anaendana na wakati uliopo kulingana na siasa za Tanzania za sasa zilivyo, aliye na uwezo wa kupambana na vyama vya upinzani kwa nguvu sana na mpaka sasa tangu ameteuliwa vyama vya upinzani nguvu yake imepungua kwa asilimia kubwa”

Diwani huyo ameitaja miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa na serikali katika Kata yao

“Miradi ambayo imepatikana Kakonko ni pamoja na mradi mradi mkubwa wa kimkakati wa stendi kubwa ya kisasa iliyochukua gharama ya Bilioni 4, ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambayo inaenda vizuri na tayari tumepata milioni 800 kwaajili ya ujenzi wa theater na monchwari na njia za kuunganisha wodi, lakini pia tumeshakamilisha wodi 3 mwaka Jana kwa milioni 750 na sasa hospitali ipo vizuri ambapo aliizindua Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan”

“Ninaamini Chama Cha Mapinduzi kimeimarika kwa asilimia kubwa” Alisema Diwani huyo.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiga Kata ya Lugenge Wilaya ya Kakonko, Petro, amesema Rais Dkt. Samia katika nyakati zake za utawaka amefanya mambo mengi ikiwemo utekelezaji miradi wilayani na ujenzi wa shule, barabara na hospitali zimejengwa vijijini

“Watanzania tuna Imani na Rais wetu kwa namna anavyoonyesha upendo wa dhati kwa wananchi wake”

Kuhusu ujio wa Makonda Kakonko amesema amekua ni mtu wa kusafisha njia ya Rais Dkt . Samia kama alivyo Yohana.

“Ukisoma Biblia makonda yeye ni Yohana, anasafisha njia ya mama na anampamba mama katika Yale anayoyafanya katika nchi yetu ya Tanzania, tunampongeza na aendelee kuisafisha njia ili tunapoelekea kwenye uchaguzi kusitokee shida yoyote”

Wakiendelea kutoa maoni, Mkazi wa Kakonko, Imelda Mathias amesema wanamategemeo makubwa na Makonda juu ya Chama chao katika kukiongoza chama kwani mwenenzi ni kama Muhubili wa Bibilia

Kuhusu kumpa kura Rais Dkt. Samia mwaka 2025, ameahidi kuwa ategemee ushindi kwani Wana Kakonko wako tayari kumpa kura zote za ndiyo.

“Tukiwa na kero RAIS Samia anakuwa wa kwanza kututatulia, ni mama mchapakazi na mpenda watu”

Juvinal Chuga, ambaye ni mkazi wa Kitongoji Cha Ukweli na uwazi, Wilaya ya Kakonko, alitefukuzwa kazi na Mkurugenzi wake mwaka 2019 mwenye umri wa miaka 56 ameupongeza ujio wa Makonda kwani ni kiongozi anayetatua kero za watu hivyo matarajio yake ni kwamba kero yake itasikilizwa na kutatuliwa kwa wakati.

“Nilifukuzwa kazi na Mkurugenzi wangu mwaka 2019, nikakata rufaa Tume ya Utumishi, Utumishi wakanizunguka, nikamwandikia RAIS, mpaka sasa hajanipa majibu, serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi kilishaelekeza wale wote ambao walitolewa kazini kimakosa warudishwe lakini mimi bado”