March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA yajizatiti kuboresha maisha ya watanzania kwa Nishati Safi na Endelevu

Na Joyce Kasiki, TimesMajira online

KATIKA kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanawafikia Watanzania wote, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuifikisha nishati salama na ya uhakika hadi maeneo ya pembezoni.

Kupitia maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, REA imeonesha kwa vitendo namna ilivyotekeleza mikakati ya serikali kwa lengo la kuinua ustawi wa wananchi, hasa waishio vijijini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Said, hadi kufikia sasa vijiji vyote 12,318 nchini vimekwishafikiwa na huduma ya umeme, huku juhudi zikiendelea kupanua huduma hiyo hadi kwenye vitongoji vyote huku akisema,hii ni hatua kubwa kuelekea kujenga Tanzania ya viwanda na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja vijijini.

Mbali na umeme, amesema REA pia imejikita kwenye kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mkakati wa taifa wa nishati safi uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2024. Mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi badala ya kuni na mkaa ambao ni hatari kwa afya na mazingira.

Amesema,katika banda lao la maonyesho ya Sabasaba, REA imeweka mfano wa teknolojia mbalimbali za nishati safi ikiwemo majiko banifu, majiko ya gesi ya gharama nafuu, na mitambo ya kutengeneza mkaa mbadala. Teknolojia hizi zina uwezo wa kupunguza matumizi ya kuni kwa zaidi ya asilimia 50 na kupunguza kwa zaidi ya asilimia 90 utoaji wa hewa chafu zinazochangia uharibifu wa mazingira na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Vile vile amesema,REA pia imeanzisha mpango wa usambazaji wa mitungi ya gesi kwa ruzuku ambapo serikali hulipia asilimia 50 ya gharama, na hadi sasa zaidi ya mitungi 452,000 inatarajiwa kugawiwa. Mradi huu, ambao sasa umefikia takriban asilimia 90 ya utekelezaji, umehusisha pia ugawaji wa mitungi 110,000 kupitia wabunge mwaka juzi.

“Kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kama Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , REA imefanikiwa kubadilisha mifumo ya kupikia katika magereza yote 129 nchini na kuanza kuwafikia askari na familia zao,aidha, shule na taasisi zinazopika kwa ajili ya watu zaidi ya 100 ni miongoni mwa walengwa wa mpango huu, ambapo mwaka huu pekee shule 53 tayari zimepatiwa huduma hiyo na lengo ni kufikia taasisi 400.

Aidha amesema,changamoto kubwa inayokabili vijiji ni upatikanaji wa huduma ya kujaza gesi mara inapokwisha. Ili kukabiliana na hilo, REA imepanga kuwezesha uanzishwaji wa vituo vya kuuza gesi na bidhaa nyingine za mafuta vijijini, ili kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi. Mfumo huu utahusisha mawakala wa kampuni za gesi ambao watapeleka huduma moja kwa moja kwa wananchi.

“REA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama wa teknolojia mpya za kupikia, kupinga dhana kwamba gesi ni hatari zaidi ya mafiga ya mawe. Mhandisi Said anasisitiza kuwa teknolojia za kisasa ni salama zaidi, hazitoi moshi, na hupunguza ajali majumbani, tofauti na mafiga ya jadi ambayo hutegemea kuni na mkaa unaoweza kusababisha moto na madhara ya kiafya.”amesisitiza Mhandisi Said

Kwa ujumla, kupitia maonyesho ya Sabasaba, REA imetoa mfano wa taasisi ya umma inayoendeshwa kwa dira, weledi na dhamira ya kweli ya kuibadilisha Tanzania. Kwa kutumia mbinu shirikishi, teknolojia bunifu na ushirikiano wa karibu na wananchi, wakala huu unaendelea kujenga msingi imara wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.