Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online Dodoma
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA),imeendelea kuhamasisha wananchi, kutumia nishati safi ya kupikia.Lengo likiwa ni kuwezesha utunzaji wa mazingira, kuboresha afya na ustawi wa jamii pamoja na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Mhandisi wa Miradi kutoka REA,Kelvin Tarimo amesema hayo,Septemba 04, 2024, jijini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha mada ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake zaidi ya 650, katika mkutano mkuu wa kwanza wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda, inayolenga kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia,” amesema Mhandisi Tarimo.
Mhandisi Tarimo,amefafanua kuwa, matumizi ya nishati isiyo safi na salama ya kupikia, huchangia uharibifu wa mazingira.Ambapo alibainisha kuwa, inakadiriwa zaidi hekari laki nne za misitu, hukatwa kila mwaka kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo matumizi ya kuni na mkaa.
Hivyo amesema kuwa,jambo hilo limekua likisababisha madhara mbalimbali ya kimazingira, ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji na ikolojia kwa ujumla.
Mhandisi Tarimo amesema katika kukabiliana na hali hiyo,REA itaendelea kuhakikisha inatimiza vyema lengo kuu la utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.
Mkakati huo,unalenga hadi kufikia Mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Hatua tunazoendelea nazo sasa ni kuongeza uelewa kwa wananchi, kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.Pia kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi kwa bei nafuu, endelevu na uhakika ya kupikia kote nchini,haswa maeneo ya vijijini na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ndogo ya nishati safi ya kupikia,” amefafanua Mhandisi Tarimo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best