June 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA yaendelea kusambaza Nishati Bora kwa wananchi,yamshukuru Rais Dkt.Samia

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

MKURUGENZI  wa Utawala wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Renatus Msangira ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake kubwa katika kuhakikisha wananchi wote nchini, hususan waishio vijijini, wanapata huduma ya umeme pamoja na nishati safi ya kupikia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2025  jijini Dodoma, katika Banda la REA kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mkurugenzi huyo amesema kuwa REA imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kufikisha umeme kwenye vijiji vyote  nchini, na sasa juhudi zimeelekezwa katika kupeleka huduma hiyo hadi ngazi ya vitongoji.

“Tumeweka umeme kwenye vijiji vingi tayari, na sasa tunakwenda hadi vitongojini. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na nishati hii muhimu,” alisema Mkurugenzi huyo.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, REA imeeleza kuwa juhudi kubwa zinaendelea ili kuhakikisha wananchi wanaachana na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa. Kupitia miradi mbalimbali, tayari majiko ya kisasa yanayoweza kutumia unit moja ya umeme kwa saa yameanza kutolewa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.

 “REA imedhamiria kuhakikisha nishati safi inamfikia kila mwananchi. Tunaendelea kugawa majiko safi na kutoa elimu kuhusu faida za kutumia nishati safi kwa afya, mazingira na uchumi wa familia,” aliongeza.

Mkurugenzi huyo amewakaribisha wananchi wote wa Dodoma na kutoka mikoa mingine kutembelea banda la REA katika maonesho hayo ili kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa, ikiwemo elimu juu ya nishati safi ya kupikia, teknolojia mpya katika sekta ya umeme vijijini, pamoja na mafanikio ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na wakala huo.

Maonesho haya yanatoa fursa kwa taasisi za umma kuonyesha huduma wanazotoa kwa wananchi, huku REA ikionyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali.