January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA Kutoa Mikopo Ujenzi Vituo vya Mafuta Vijijini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imekuja na mpango wa kutoa mikopo midogo kwa ajili ya kujenga vituo vya mafuta vidogo vidogo vijijini ili kuzuia ajali za moto zinazotokana na kuuza mafuta ya Petroli kwenye madumu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati wa hafla ya uwashaji wa umeme wa REA Jimbo la Geita Mjini, mkoani Geita leo Oktoba 2, 2023.

“Tumekuja na mpango wa kuwapa watu mikopo midogo, tuanzishe vituo vya mafuta vidogo vidogo vijijini ili watu wetu waache kuuza madumu ya Petroli humu, na baadae wanapata ajali ya kuunguzwa na mafuta hayo,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Vilevile amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inagawa mitungi ya gesi kwa ruzuku ndogo ili kuwasaidia Wanawake Watanzania kupika kwa kutumia nishati hiyo mbadala.

“Rais anapenda wanawake Watanzania, ameyaona mateso yao ya kupika kwa kutumia kuni, tumekuja na nishati mbadala ya kuwasaidia Wanawake wa Tanzania wapike kwa kutumia nishati mbadala,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Wakati huo huo Mhe. Dkt. Biteko amewaomba viongozi wote waliochaguliwa na kuteuliwa kusimamia miradi ya Serikali na fedha zote zinazoletwa ziwahudumie Watanzania.

“Hakuna maana yoyote, sisi viongozi kuwa tunaishi maisha ya mjini lakini wananchi wetu wa vijijini hali zao ngumu. Mhe. Rais anatoa fedha kwa ajili ya watu hawa, anatoa fedha anajima, anapambana kwa ajili ya maendeleo ya watu, anataka kuona wananchi wanahudumiwa,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Hivyo ametoa wito kwa viongozi wote, kuhudumia wananchi masikini wanaotaka kujipambanua kupata maendeleo yao.

Naye, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 39.1 kwa ajili ya kuweka umeme vijiji vyote vya Mkoa wa Geita ambavyo havijpata umeme.
 
Aidha ametaja miradi mitatu inayoendelea kutekelezwa katika Jimbo la Geita Mjini kuwa ni Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Kupeleka umeme Pembezoni mwa Miji pamoja na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.