Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umechukua hatua za kimkakati, ikiwemo ujenzi wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme kwa lengo la kupunguza changamoto ya kukatikakatika kwa umeme nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy, ametoa kauli hiyo Leo Januari 15,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma Kufuatia uzinduzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Mtera unaotarajiwa kufanyika Januari 16,2026 huku Waziri wa Nishati Deo Ndekembi akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio Hilo.
Mhandisi Saidy alisema hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji na uhakika wa umeme katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa pamoja na mikoa ya Dodoma na Iringa kwa ujumla.
Alisema uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati Vijijini unaolenga kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wote bila kujali wanakoishi.
Ameeleza kuwa kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 9.7, fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali za Sweden na Norway. Kukamilika kwa mradi huo kumechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la umeme hafifu, kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuimarisha usambazaji wa umeme kutoka Mtera kwenda Dodoma na Iringa.
Mhandisi Saidy ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho umehusisha ufungaji wa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 10 kila moja, chumba cha switchgear kwa ajili ya mifumo ya umeme, pamoja na mifumo ya udhibiti na mawasiliano.
Amefafanua kuwa miundombinu hiyo itaongeza uwezo wa TANESCO katika kusambaza umeme kwa ufanisi zaidi kwa wananchi, viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Katika hatua nyingine, alisema REA inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji zaidi ya 9,000 kote nchini. Tangu mwaka 2021 hadi sasa, vitongoji 28,000 tayari vimeunganishwa na umeme, huku vitongoji 13,445 vikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya takribani shilingi trilioni 1.2 na unatarajiwa kutoa ajira zisizopungua 4,600 moja kwa moja kwa wananchi wa vijijini.
Aidha, Mhandisi Saidy alisema REA ina mpango wa kujenga vituo vidogo vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mtwara, Hanang, Nzega na Mbarali, ambapo taratibu za awali za utekelezaji zinaendelea. Lengo ni kuhakikisha kila wilaya nchini inakuwa na kituo cha kupoza umeme ili kuongeza uhakika wa huduma hiyo.
Ameongeza kuwa miradi hiyo itawezesha kuunganishwa kwa miundombinu muhimu ya kijamii ikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na pampu za maji, hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijijini. Pia amewahimiza wananchi kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme kuboresha maisha yao na kukuza shughuli za uzalishaji.
Kwa upande mwingine, aoisema REA inatarajia kusaini mikataba ya utekelezaji wa mradi mwingine wa kupeleka umeme kwenye vitongoji takribani 9,000 kote nchini.
Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Januari 17, 2026 katika Ukumbi wa Hazina Ndogo jijini Dodoma. Mradi huo utatekelezwa kupitia mafungu 30 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Aidha Mhandisi Saidy alisema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia Watanzania wote na kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama