January 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Tanga akutana na Mtendaji Mkuu Air Tanzania na kufanya mazungumzo

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga amekutana na Mtendaji mkuu wa shirika la ndege la Air Tanzania ili kuangalia uwezekano wa namna shirika hilo linavyoweza kukitumia kiwanja cha ndege cha Tanga kwenye safari zake.

Akizungumza kwenye kiwanja hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akifuatana na mtendaji mkuu wa Air Tanzania, amesema serikali inaangalia namna ya kuupanua uwanja huo ili uweze kuhudumia ndege kubwa kutoka maeneo mbalimbali.

Malima amesema kwamba Tanga ni moja ya mikoa yenye biashara kubwa hususani kwa wasafiri wa ndege kwani wapo watu wanaotamani kutoka Tanga asunuhi na kwenda kufanya shughuli zake maeneo mengine na jioni kurejea.

“Sisi tunataka kuwa kupokea ndege kubwa hapa Tanga niwaombe Air Tanzania kuwa watumiaji wa kubwa wa kiwanja hiki pale tutakapofikia lengo hilo kwani sasa ivi uwanja una mita 1250 ili kiwanja kiwe comfortable kwajili ya kutua bombadier na sisi hapa tuko kwenye usawa wa bahari tukipata mita 1700 hatuko vibaya, “alisema RC Malima.

Naye mtendaji mkuu wa shirika la ndege la Air Tanzania Ladislaus Matindi amesema shirika hilo liko tayari kuanzisha safari za Tanga mara baada ya mpango wa upanuzi wa kiwanja hicho kukamilika.

Matindi amesema kuwa Tanga ni moja ya sehemu ambayo wamekuwa wakihudumia kwa miaka iliyopita huku teknolojia ya viwanja na matakwa kubadilika hivyo kwa ndege waliyonayo hivi sasa ya kiwanja kuwa kifupi hakiwezi kuhimili uwezo wa ndege walizonazo.

“Tayari hilo wazo la kusema tupanue huu uwanja hasa hii njia ya kurukia ndege runway iweze kuwa na uwezo wa kuhudumia hizo ndege zetu na sababu ipo kubwa tuu kwa kuwa mzunguko hasa wa kibiashara Tanga ni mkubwa hivyo tatizo ni la miundombinu ti ambalo serikali tayari imeliona, “alisistiza Mtendaji Matindi.

Meneja wa kiwanja cha ndege mkoani Tanga Mussa Mcholwa akisema jambo hilo litasaidia kuongeza fursa za kibiashara na kiuchumi.

“Ndege kubwa saizi ya kati zitatua mzunguko utaongezeka, sababu kama bombadier Q4100 inabeba abiria 80 kwahiyo mnaweza mkaona kutoka abiria 12 kwenye caravan mpaka abiria 80 kwahiyo kwa sisi mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania tutaongeza, mapato pindi kiwanja hichi kitakapopanuliwa alibainisha, ” Meneja huyo.

Serikali inaangalia mpango wa namna ya upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mkoani Tanga ili kukijengea uwezo wa kutumiwa na ndege kubwa za abiria.

Mpango wa serikali ni kupanua kiwanja hicho kutoka mita 1250 zilizopo hivi sasa hadi kufikia mita 1700 ambazo zitawezesha ndege kubwa kuweza kutua.