January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Songwe atoa maelekezo mahususi magari ya wagonjwa

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dkt.Francis Michael, ametoa maelekezo mahususi kwa Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo, kuhusu magari ambayo yametolewa na serikali kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za afya na kubebea wagonjwa.

Dkt.Francis ametoa maelekezo hayo leo Februari 20,2024, wakati akikabidhi magari 10 kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo, kwa ajili usimamizi wa shughuli za afya na kubebea wagonjwa katika maeneo yao.

Amewata Wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa magari hayo kwenda kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si kwenda kufanya shhughuli nyingine.

“Hatutarajii kuyaona magari ya wagonjwa yakitumika kwa shughuli nyingine tofauti na kusafirisha wagonjwa” alisisitiza Mkuu wa Mkoa Dkt. Francis.

Vile vile Wakurugenzi hao wa Halmashauri wametakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya kufanya matengenezo endelevu ya magari hayo ili kuepusha kuchakaa mapema na kushindwa kufanya kazi.

Aidha,amezitaka timu za usimamizi wa huduma za afya katika mkoa huo nazo kuhakikisha kuwa zinayatumia vizuri magari hayo, ili kukabiliana na changamoto vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga vinavyotokea kutokana na kuchelewa kusafirishwa kutoka vituo vya ngazi ya chini kwenda kwenye vituo vinavyotoa huduma za dharura.

Dkt. Francis alieleza mgawanyo wa magari hayo 10 yaliyopokelewa mkoani hapo kuwa, magari manne ni kwa ajili ya shughuli za usimamizi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, pamoja na timu za usimamizi za Wilaya za Songwe na Ileje.

Aliongeza kuwa, magari sita yatapelekwa katika kila jimbo kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe na kwamba Mkoa huo bado unatarajia kupokea magari mengine matatu kwa ajili ya timu za usimamizi katika Halmashauri za Wilaya za Mbozi na Momba, pamoja na Halmashauri ya Mji Tunduma.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt.Boniphace Kasululu, alisema kuwa kabla ya mkoa huo kupokea magari hayo 10,Mkoa huo ulikuwa na magari 13 tu ukilinganisha na mahitaji halisi ya magari 30 kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa huduma za afya na kubebea wagonjwa.