Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Songwe
MKUU wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, amesema muda si mrefu Songwe itakuwa kinara katika kutekeleza kampeni ya usafi wa mazingira, kwa kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo unaenda kufanyika kwa kasi na ufanisi mkubwa.
Brigedia Jenerali Mwangela ameyasema hayo mara baada ya kutembelea vijiji vya Halmshauri ya Wilaya ya Njombe ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuona namna walivyotekeleza kampeni ya usafi wa mazingira kwa ufanisi na kuongeza kuwa sasa amebaini siri ya mafanikio yao.
“Nimeona na nimejua siri yao na sasa tumejifunza mengi tunaenda kutekeleza kampeni hii kwa kasi kubwa, tutawashirikisha tuwape elimu wananchi, viongozi wa dini na wa Serikali ngazi zote, kila mmoja aweze kuhusika kikamilifu ili wote tuibebe kwa pamoja kampeni hii,” amesema Brigedia Jenerali Mwangela.
Ameongeza kuwa katika kutekeleza kampeniya usafi wa mazingira kwa ufanisi watahakikisha wale wasio na uwezo na hawana ndugu wanawekewa utaratibu wa kusaidiwa na uongozi wa vijiji na mitaa ili kila kaya iwe na choo bora na kuweka sheria ili kuwabana wachache watakao kaidi.
Hata hivyo amesema Songwe haifanyi vibaya sana katika usafi wa mazingira, bali utekelezaji wa kampeni hiyo unapaswa kufanyika kwa kasi zaidi na ufanisi.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Dkt Seif Shekalaghe amesema kampeni ya usafi wa mazingira ni ajenda ya kitaifa ambayo ina mipango mikakati inayotumika maeneo yote, hivyo wamefanya ziara kujionea namna Mkoa wa Njombe ambao unafanya vizuri kitaifa umetekelezaje mipango hiyo.
Dkt. Shekalaghe amesema wamejifunza kuwa Njombe wamefanikiwa kwa kuwa walitekeleza kampeni ya usafi wa mazingira kwa ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi ya chini.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Matiganjola wilayani Njombe, Erasto Joseph Kapinga amemuambia Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuwa wana kijiji wote walipewa elimu ya usafi wa mazingira na mafanikio ya kampeni hiyo ni pamoja na kutokuwepo kwa magonjwa ya tumbo na kuharisha kijijini hapo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba