Na Anthony Ishengoma,Timemajira Online, Shinyanga
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati amesema hatakuwa mvumilivu kwa viongozi na watumishi wa umma watakaoshindwa kusimamia na kusababisha kuzorota kwa maendeleo mkoani hapa.
Dkt. Sengati ameyasema hayo jana wakati akiwakaribisha Wakuu wa Wilaya wapya wa Kishapu na Kahama, waliofika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kujitambulisha mbele yake lakini pia, mbele ya wadau mbalimbali wa walioko Mkoa wa Shinyanga.
‘’Sitavumilia, nitahakikisha natumia mbinu zote kuhakikisha wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za kiutumishi, lakini pia hatua za kinidhamu kwa sababu Watanzania ni wengi wenye uwezo wa kuwahudumia wananchi,’’ amesisitiza.
Amewataka Wakuu hao wa Wilaya, kufanya tathmini ya kina ili kuja na mikakati ya kuiendeleza Shinyanga kama mkoa wa kimkakati na inayoendana na Tanzania ya uchumi wa kati, lakini pia ulimwengu wa kidijitali ili kuthibitisha kuwa wao ni viongozi wa karne ya Sayansi ya na Teknolojia.
‘’Napenda kuona mahusiano makubwa ya utajiri wa mkoa wetu na ubora wa maisha ya wana Shinyanga, natamani kilimo, madini na mifugo takribani milioni nne, biashara kubwa na uwekezaji ulioko Shinyanga, uhakisiwe katika ubora wa maisha ya watu wa Shinyanga,’’ amesisitiza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu aliyemaliza muda wake, Nyamaganga Taraba akitoa maoni yake wakati wa kuaga wajumbe wa mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo fupi, amesema mtu akiona ameteuliwa ajue kuna kazi anayokwenda kufanya na akiona ametenguliwa ajue kuna kazi amekamilisha.
Amesema kazi waliyotumwa wameikamilisha kwani wameiacha Shinyanga ambayo si jangwa tena, wamepunguza tatizo la mimba na ndoa za utotoni lakini pia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwaomba viongozi wapya, kuendeleza yale mazuri waliyoyaacha na kuwataka kuendana na watu wa Shinyanga ambao ni wasikivu wanaotaka kuendana nao sawa.
Wakati huo huo Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga ameahidi kuja na mkakati wa kupunguza umaskini kwa watu wenye maisha duni na kuweka mikakati itayowainua maisha yao, ili waweze kujiona na wao wana nguvu ya kuendana na soko la kiushindani lililopo.
‘’Unapomwondoa mtu katika umaskini, maana yake unataka naye awe sehemu ya nguvu ya soko na awe na uwezo wa kununua na hivyo aweze kuchangia katika ujenzi wa uchumi, tunataka Kahama inayokuwa na nguvu kubwa ambayo kila mmoja anaweza kuingia sokoni,” amesema.
Hivi karibuni Serikali ya awamu ya sita, imefanya mabadiliko katika uongozi wa wilaya mbalimbali nchini na katika mabadiliko hayo, Mkoa wa Shinyanga ulipata madiliko ya viongozi hao kwa wilaya zake mbili za Kishapu na Kahama.
More Stories
Kapinga asema mafanikio katika sekta ya nishati yanatokana na jitihada za Rais Samia
Bumbuli kutekeleza miradi kwa kuangalia vipaumbele
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi