November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Nchimbi aipongeza WMA, aagiza elimu ya vipimo kwa watendaji wote

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Singida

MKUU wa MKoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, amepongeza Wakala wa Vipimo (WMA) kwa kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya vipimo na ufungashaji kwa mkoa huo na ameagiza viongozi wa mkoa kuhakikisha unafanyika utaratibu ili wataalam na watendaji wote wanaohusika na wazalishaji wapate mafunzo hayo yanayohusiana na vipimo.

Dkt. Nchimbi alitoa kauli hiyo mkoani Singida jana wakati akifungua mafunzo na elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya vipimo na ufungashaji, ambayo yaliwashirikisha wafanyabiashara wanaosindika mafuta na kufungasha bidhaa mbalimbali.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na WMA. “Ninawapongeza WMA kwa kutoa mafunzo haya hapa kwetu na ninamuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida na wakuu wa wilaya zote kuhakikisha unafanyika utaratibu wa wataalam wote wanaohusika na wazalishaji kupata mafunzo haya,” amesema na kuongeza;

“Nataka kuona darasa la namna hii juu ya vipimo kwa watendaji wote, wakiwemo maofisa ugani, lazima wawe na majibu kuhusu vipimo.”

Ameagiza Sekretarieti ya mkoa huo na za wilaya kuhakikisha mafunzo hayo yanatolewa katika maeneo yao na kwamba katika hilo, hakuna bosi.

“Bosi ni mzalishaji na yule anayetaka vifungashio vilio sahihi na tunaowatumikia ni wale wanaozalisha, wanaotafuta vipimo sahihi, wanaotafuta kuwa na vifungashio vilivyo sahihi,” amrsema na kusisitiza;

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Dkt, Adelhelm Meru akizungumza na Kaimu Ofisa Mtendaji wa WMA, Stella Kahwa wakati wa mkutano wa 29 wa Baraza la Wafanyakazi wa WMA uliokuwa na lengo la kujadili Mpango na Bajeti katika Kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 wiki iliyopita. Picha na Mpiga picha wetu.

“Wazalishaji mkizalisha vizuri mkatumia vipimo sahihi na kuweka katika vifungashio vilivyo na ubora, ndipo kutasaidia kuwepo uchumi uchumi imara.”

Amesema muda sio mrefu anataka kuona mafunzo hayo kwa watendaji wote na yeye akiwemo na kwamba katika hilo hakutakuwa na visingizio.

“Haiwezekani wawepo watendaji, watumishi na watalaam ndani ya mkoa na wilaya zetu halafu, tumsubiri mtu wa WMA kutoka Dar es Salaam au Dodoma kutupa mafunzo,” ameonya na kusisitiza;

“Ni lazima tujitosheleze kikamilifu kwa kila kitu.” Amewaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa vipimo sio kitu cha mzaha katika maisha ya binadamu, kwani vinajenga kujiamini na kujua jinsi ya kutengeneza kitu kilicho bora kwa kutumia vipimo.

Amesema vipimo ndivyo vinamfanya mzalishaji ajue kuwa ametoka kwenye uzalishaji wa kilo tatu na kufikia kilo 20. “Kwa hiyo vipimo vinakuwezesha kujua mwendo wako katika safari yako ya uzalishaji, vinajenga imani, kujiamini na kuaminiana.”

Ameendelea kufafanua kwamba; “Pamoja na sheria, kanuni na taratibu za nchi, tunataka wazalishaji wetu wawe na amani, wajiamini, wafurahie uzalishaji wao na hawawezi kufurahia iwapo hautasimama au kuoneshwa na vipimo. Vipimo ni sehemu ya uzalishaji.”

Amesisitiza kwamba vipimo ni kiashiria cha haki na ni sehemu ya maisha yao katika suala zima la uzalishaji kwa Mkoa wa Singinda.

Dkt. Nchimbi amesema kama una vipimo vizuri, utadhihirika katika utendaji wako wa kila siku na mwisho wa siku tija itakayopatikana itakuwa ni ya mkoa.

Ametoa pongezi kwa wote ambao wameshiriki mafunzo hayo, akisema suala zima la taarifa kuhusiana na vipimo, sio suala la msimu, bali ni hitaji la kila siku.

“Kwa hiyo hatuwezi kusubiri mtu anayetoka Dar es Salaam atuletea taarifa za vipimo, vipimo havitekelezwi ofisini, bali vipo kwa wananchi, wazalishaji. Utaalam wa ufungashaji hauko ofisini na wanaotaka kuona thamani ya vifungashio hawapo ofisini,” amesisitiza.

Rumbisa ya vitunguu; Ufungashaji wa aina hii unapigwa marufuku na WMA kwani unamwibia mkulima na uzingatii sheria

Amesema wanataka kuona kwamba Singida ambayo haitumii vipimo imekwisha. Amesema Singida wanayoitaka ni ile inayotaka vipimo sahihi na vipimo bora.

Amesema haisaidii kumchukulia mtu hatua za kisheria, eti kwa sababu hakuzingatia vipimo , bali wanataka anufaike na uzalishaji wake kwa kuzingatia vipimo vilivyo bora, ndiyo maana watendaji wawe na elimu hiyo waweze kuwashauri na kuwafuatilia wazalishaji wakati wote wa uzalishaji na uuzaji.

Amesema hilo wataanza nalo na watajipima wenyewe kama mkoa ili kujua wamefanikiwa kwa kiasi gani na kama ni adhabu, watajipa wenyewe kama Serikali ya mkoa.

Alisema uamuzi wa WMA kutoa mafunzo hayo Singida umedhihirisha kwamba Singida ni ya uzalishaji uliotukuka.