Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online,Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatuma Mwasa, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kwa kupata hati safi na hoja chache kuliko halmashauri zote.
Hajat Mwasa, amesema hayo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Amesema miaka mitatu ijayo Manispaa hiyo itakuwa imeimarika zaidi ikiongeza kasi ya kukusanya mapato ya ndani.
Pia amesema Mkurugenzi na Watumishi wote waanze mkakati wa kuzuia hoja kwa sababu zikibuka maana yake wamekiuka taratibu na miongozo iliyopo.
Huku akitole mfano wa hoja iliyojitokeza ya miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 2.1ambayo haijakamilika.
Hata hivyo amewataka pia kuzingatia thamani ya fedha na miradi inayoibuliwa ya maendeleo.
Ambapo ameeleza kuwa changamoto ni mapato ya ndani kuwa madogo kwa sababu mikoa mingine fedha za miradi kutoka serikali kuu ikichelewa huwa wanatumia mapato hayo.
Hivyo amewataka wahakikishe wanaongeza mapato ya ndani ili kuweza kumalizia miradi viporo.
Amesema jukumu kubwa katika kukusanya mapato ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara ambapo hizo milioni 432 ambazo hazikukusanywa zingesaidia katika miradi ya maendeleo.
“Hatuwezi kufanya maendeleo bila kukusanya kodi hata wafanyakazi tunakatwa kodi asilimia 30 ya mishahara yetu,”amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Awali akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa niaba ya Mkurugenzi Mwekahazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Flora Lengwana,amesema jumla ya hoja zilizoibuliwa ni 21 kati ya hizo 4 zimetoka miaka ya nyuma na hoja 17 ni mpya .
Lengwana,amesema hoja zilizojibiwa kikamilifu ni 12 na hoja 9 utekelezaji wake unaendelea huku zinazoendelea ni pamoja na mfumo wa ukusanyaji mapato kutokuwa sawa,mapungufu katika kuibua vyanzo vya mapato ya ndani,mapungufu katika mfumo wa tehama ( watumishi wa tehama kutopata mafunzo).
Amesema hoja zingine zinazoendelea pia kutokukamilika kwa miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 300 ambapo Mkaguzi amemshauri Mkurugenzi kuitengea bajeti ya kukamilisha.
Amesema miradi ya miaka ya nyuma ambayo imetelekezwa bila kukamilika yenye thamani ya bilioni 2.22 ambayo haijakamilika waitafutie fedha na kuikamilisha ili isiendelee kuibua hoja kila mwaka.
Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Steven Ndaki,amewataka kuanzisha mkakati wa kuzuia hoja katika Manispaa hiyo na kuwa makini katika kila hatua za kutekeleza miradi ya maendeleo na kuibua vyanzo vipya vya mapato ya ndani bila kuibua hoja zisizokuwa za lazima.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Jacob Nkwera ,amesema hoja zote zilizoibuliwa na Mkaguzi atazipatia ufumbuzi ambapo mwaka wa fedha ujao miradi viporo ya maendeleo imepewa kipaumbele.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba