November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Mtanda awapa shavu waandishi wa habari

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

SERIKALI mkoani Mwanza,imeahidi ushirikiano na
vyombo vya habari na kuziagiza taasisi zake kuhakikisha zinatoa habari
zinazotakiwa na waandishi wa habari.


Pia imewataka wanahabari hao kuandika habari zilizofanyiwa
utafiti na kuzichakata kwa maslahi ya nchi na maendeleo ya wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa Aprili 8,2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,wakati akizindua kongamano la uchumi wa buluu na maonesho ya picha lililoandaliwa na TMFD lililofanyika jijini Mwanza.

Mtanda amesema anatambua viongozi wa serikali walio wengi ni
wagumu kutoa habari wanazozihitaji waandishi wa habari,hivyo mkoani Mwanza atasimamia
wazitoe na wazipate kwa wakati.

“Waandishi wa habari wanatakiwa kutendewa haki,wana
mchango katika kukuza uchumi,maendeleo,kudumisha amani na utulivu wa nchi,pia nafahamu
changamoto zao,taasisi za umma zinazowatumia nitahakikisha wanapata haki na
maslahi bora (posho),”amesema Mtanda.

Ameeleza kuwa uhuru wa waandishi wa habari mkoani Mwanza atahusika
nao,hakuna atakayekamatwa kwa kupotosha badala yake atakuwa tayari kutoa ufafanuzi
wa upotoshaji huo na kuwataka kuandika ukweli kwa kuzingatia miiko ya taaluma
yao.

“Andikeni ukweli kwa maslahi ya taifa na Mkoa wetu,nitatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha tasnia yenu haipati kikwazo mkoani Mwanza na mwandishi wa habari hatakamatwa kwa kupotosha,”amesema Mtanda.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazitumie kalamu zao kwa weledi zisisababishe migororo,zikitumika
vibaya zinaweza kuzorotesha amani na utulivu,hata kukwamisha maendeleo kwani kwenye vurugu hakuna maendeleo.

“Watu wa kweli walioongoka na wanaotaka maendeleo nitafanya nao kazi,wababaishaji sitakuwa na nafasi nao wenye mambo ya
majungu,migogoro na kufitinisha,”ametahadharisha Mtanda.


Aidha,amewataka kuwa huru
katika kupata habari na wenye wajibu wa kuimarisha amani ya Mkoa na utulivu.