March 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Mtanda ataka uchunguzi wa haraka ajali ya moto soko la mbao Sabasaba 

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza 

Ajali ya moto ambayo chanzo chake akijajulikana kimeteketeza mali ya baadhi ya wafanyabiashara katika soko la mbao la Sabasaba wilayani Ilemela mkoani Mwanza huku  Mkuu wa Mkoa huo Said Mtanda,akiagiza uchunguzi kufanyika haraka ili kubaini chanzo cha moto huo.

Kwa mujibu wa  Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, SSF. Elisa Kamugisha, amesema moto huo ulianza majira ya saa saba usiku kuamkia Machi 17,2025, na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuuzima mapema  ili usienee sehemu nyingine.

“Hapa kuna wafanyabiashara wa mbao zaidi ya 1000,lakini walioathirika na ajali hii ya   moto ni 30,lakini taarifa rasmi itatolewa muda siyo mrefu,”amesema SSF. Kamugisha.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, akizungumza Machi 17,2025, alipowatembelea wafanyabiashara wa mbao katika soko hilo  la Sabasaba,ambako ajili ya moto imetokea mbali na kuwapa pole  amewataka kuwa watulivu wakati   uchunguzi wa chanzo cha moto huo ukiendelea kufanyika.

Mtandao,amesema mara baada ya uchunguzi  kukamilika na taarifa kusomwa,ofisi yake  itakutana na wafanyabiashara hao pamoja na taasisi za fedha, ili kuona namna ya kuwapa muda zaidi wa marejesho  kwa wale waliokopa.

“Natoa rai kwa vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi huu ili kutambua chanzo moto,na kujua nini kifanyike na wafanyabiashara hao waendelee na shughuli zao mapema iwezekanavyo kama Serikali inavyohimiza wananchi kuwajibika,”amesema Mtanda.

Sanjari na hayo  amewataka wafanyabiashara hao, kuzingatia matumizi ya vifaa vya kuzimia moto na bima, ambayo itawasaidia kuepuka hasara kubwa yanapotokea majanga ya moto kama hilo. 

Amesema,mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na moto huo,amepata taarifa kuwa  idadi kubwa ya wafanyabiashara hao hawatumii vifaa vya kuzimia moto licha ya elimu ya matumizi hayo kutolewa mara kwa mara na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Kuna maeneo ya majanga, Serikali inawajibika moja kwa moja kuwagharamia wananchi na mengine haiwajibiki kama hili,nawakumbusha kuzingatia sheria zinavyotaka ili kujihakikishia usalama  muda wote wa mali zenu.Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  mmefanya kazi hii kwa weledi na kuokoa sehemu kubwa ya mali za wafanyabiashara hawa,”amesema Mtanda.