Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.
MKUU wa Mkoa wa Mara,Kanali Evans Mtambi, amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya ‘Mara Day’ ambayo yanashirikisha nchi ya Kenya na Tanzania.
Maadhimisho ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 15, 2025, katika Viwanja vya Mwenge, Wilaya ya Butiama.
Tarehe ya maadhimisho ya Mara Day inahusiana na tukio la wanyama (nyumbu) kuhama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania kwenda Maasai Mara, Kenya kwa ajili ya kutafuta malisho na kuzaliana, kisha kurejea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Hifadhi hii imeweza kuwa bora kwa vipindi viwili tofauti mfululizo na kuipa heshima nchi ya Tanzania.
Kanali Mtambi ameyasema hayo leo, Septemba 11, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Musoma. Amesema kuwa maonesho hayo ni ya 14 na ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla kuvitangaza vyema vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani hapa, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Bonde la Mto Mara.
Aidha, amesema kuwa shughuli mbalimbali zitafanyika katika maadhimisho hayo, ikiwemo kupanda miti takribani 8,000 katika Kijiji cha Kirumi, Wilaya ya Butiama, kufanya maonesho ya teknolojia mbalimbali zinazotumika katika masuala ya uhifadhi, pamoja na michezo mbalimbali.
Shughuli nyingine ni mijadala na makongamano ya kisayansi, usimikaji wa vigingi 50 kubainisha mipaka kati ya Bonde la Mto Mara na wananchi wa Kijiji cha Kirumi, kusudi wajue mipaka yao ili kuepusha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya Bonde la Mto Mara, pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi wa Mto Mara kwa vijiji 136 vinavyopakana na bonde hilo.
Kanali Mtambi amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kutoa msukumo wa kufanyika kwa uhifadhi wa Bonde la Mto Mara, ambalo linaanzia milima ya Mau nchini Kenya na kuishia Ziwa Victoria nchini Tanzania. Amesisitiza kuwa bonde hilo ni chachu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hivyo lazima juhudi ziendelee kufanywa kuhakikisha linazidi kuleta tija.
Aidha, Kanali Mtambi amesema kuwa uamuzi wa Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria, uliofanyika Mei 4, 2012 Kigali, nchini Rwanda, ulielekeza kufanyika kwa maadhimisho ya Mara Day kwa kupokezana kati ya Kenya na Tanzania.
Hivyo, maadhimisho hayo yameendelea kufanyika kila mwaka Septemba 15, huku yakiwaleta pamoja viongozi, wadau, wananchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa kushiriki katika jambo hili muhimu.
Mussa Paulo ni Mkazi wa Kata ya Nyasho Manispaa ya Musoma, amesema ili bonde la Mto Mara Liwe endelevu Wananchi wanalojukumu la kutojihusisha na shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima kando ya bonde hilo.
James Shaban Mkazi wa Kitaji Manispaa ya Musoma amesema elimu inapaswa kuzidi kutolewa kwa Wananchi wote kuhusu faida za bonde hilo, mikakati madhubuti ambayo ni shirikishi izidi kufanywa kuondoa athari katika bonde la mto Mara ambalo ni muhimu kwa viumbe hai na uchumi kupitia sekta ya utalii.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama