Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Mara
MKUU wa Mkoa wa Mara Kanali Evance Mtambi amekemea tabia ya watumishi wa serikali na taasisi za umma mkoani humo ambao wamekuwa kikwazo cha utoaji wa taarifa sahihi kwa Waandishi wa Habari kuacha tabia hiyo.
Amesema, hakuna sababu ya kushindwa kuwapa taarifa na ushirikiano Waandishi wa Habari wanapowafikia kwa lengo la kupata taarifa ili kuuhabarisha umma.
Kanali Mtambi ameyasema hayo Mei 17, 2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari kimkoa yaliyofanyika Mjini Musoma ambapo amesema kutokana na serikali kufanya maendeleo ambayo yanaonekana wazi na kama kuna changamoto waziseme bila uficho kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.
“Natoa onyo kwa Watumishi wa serikali na Taasisi za umma wanaowanyima taarifa Wanahabari waache tabia hiyo. Hakuna haja ya kuwanyima taarifa Waandishi wa Habari, Waandishi ni kioo cha Jamii kama kuna kiongozi anawaona ni kero basi anamatope na ni vyema aongeze uwajibikaji katika eneo lake haiwezekani uwafiche mambo ambayo wakiyaandika yanafaida kwa jamii.”amesema Kanali Mtambi na kuongeza.
“Niwatake pia viogozi mkoani Mara wanaowabedha ama kuwadharau Waandishi wa Habari ama kuwatisha waache kusudi wafanye kazi yao kwa uhuru pia Waandishi mtambue mipaka yenu katika utekelezaji wa kazi zenu huku mkizingatia weledi na maadali ya taaluma yenu, kusudi jamii ipate taarifa sahihi zenye kuleta mabadiliko na kuchochea maendeleo,”amesema Mtambi.
Aidha, amewataka kuutangaza vyema Mkoa wa Mara na rasilimali zake kusudi zitumike kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa huo sambamba na kutumia kalamu zao kukemea matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya ukatili,wananchi kujichukulia sheria mkononi na matukio yote yanayokinzana na sheria za nchi.
Kwa upande wake Ofisa Mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Musoma Fikiri Kenyera amewaomba waandishi wa habari ndani ya Mkoa wa Mara kusaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji mazingira ikiwemo kuhimiza upandaji wa miti, kuachana na tabia zisizozingatia uhifadhi wa mazingira ikiwemo ukataji miti na shughuli za kibinadamu zenye madhara.
“Tunashuhudia mabadiliko ya tabia nchi na madhara yake ikiwemo mafuriko baadhi ya maeneo, ukame na majanga mbalimbali,toeni elimu kupitia makala, habari na kuendesha vipindi redioni vinavyowaleta pamoja wadau kulinda na kuhifadhi mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”amesema Kenyela.
Awali Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara Raphael Okello, amesema Mkoa huo una waandishi wa habari wapatao 60 na klabu hiyo imeendelea kusimamia maadili na weledi kwa waandishi hao ili wazingatie maadili ya kazi yao.
Amesema, jumla ya vyombo 17 vya habari vinamilikiwa na waandishi ndani ya Mkoa huo na vimekuwa chachu ya kuleta maendeleo na kuwa daraja kati ya serikali, wadau na jamii huku akisema kuwa klabu hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wote mkoani humo ili kuimarisha uwajibikaji wa pamoja.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato