January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mrindoko:Vyombo vya haki jinai shirikianeni kumaliza kesi kwa wakati

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

VYOMBO vyote vya Haki Jinai vimeombwa kushirikiana kwenye masuala ya uendeshaji wa kesi kwa kuzingatia sheria,kanuni, taratibu ili kurahisisha uendeshaji wa kesi mbalimbali.

Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko,ametoa rai hiyo Januari 01, 2025 huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa vyombo vya haki jinai utasaidia kumaliza kwa wakati kesi ambazo hazihitaji muda mrefu kusikilizwa na kutolewa hukumu.

Akiwa katika Gereza la Mahabusu Mpanda wakati wa sherehe za mwaka mpya 2025, Mrindoko ameweka wazi kuwa idara hiyo ya magereza inafanya kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayowapa mafunzo wafungwa watakapotoka waweze kuwa raia wema.

Utekelezaji wa miradi mbalimbali umelenga kutoa mafunzo kwa wafungwa hususani wakati watakapo maliza vifungo vyao waweze kuwa raia wema na wenye uwezo wa kufanya kazi.

Kiongozi huyo wa mkoa, Mbali na hayo ameipongeza Magereza kwa kuendelea kusimamia mahabusu pamoja na wafungwa ambao wanahifadhiwa gereza hilo la mahabusu.

Mrindoko katika hatua nyingine ametoa mbuzi wanne kwa ajili ya nyama na vinywaji baridi kwa mahabusu na wafungwa.

Akimkabidhi zawadi hizo Mratibu wa Gereza la Mahabusu Mpanda Fred Mwakatobe, amesema mwaka 2025 uwe mwaka mwema wa kila mmoja huku Wafungwa na Mahabusu na Askari  magereza waweze kushikwa mkono zaidi waendelee kuwalea vyema.

Mratibu huyo wa gereza la mahabusu, licha ya kumshukuru mkuu wa mkoa wa Katavi kwa zawadi ya mwaka mpya kwa wafungwa na mahabufu amesema ni jambo jema ambalo limewafanya kujisikia ni sehemu ya jamii japo kuwa wamefungwa.