January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Michael ataka mwanafunzi aliyekatisha masomo kurejeshwa shuleni

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Ileje.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dkt.Francis Michael, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Frida Mgomi kuhakikisha anamrejesha shuleni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya wasichana (Ileje Girls) anayedaiwa kukatisha masomo na kwenda kufanya kazi za ndani ili aendelee na masomo.

Pamoja na hilo, Dkt. Michael ameagiza
Kurejeshwa shuleni hapo kwa wanafunzi wengine watatu ambao wazazi wao
waliwahamisha na kuwapeleka katika shule za kutwa kwa kisingizio cha wazazi hao kukosa michango ya chakula.

Dkt. Michael,ametoa maagizo hayo November 14, 2023, wakati akitimiza ahadi yake ya kuwapatia kila mwanafunzi madaftari tano (Counter book) wanafunzi wote wa shule hiyo.

Awali akitoa taarifa ya shule, Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Sharon Kadinde, amesema kuwa shule hiyo ya wasichana iliyoanzishwa mwaka huu ilipangiwa wanafunzi 75 , lakini walioripoti shuleni hapo ni 71 tu.

Ameongeza kuwa mwanafunzi mmoja alikatiza masomo kwa shinikizo la wazazi wake, huku wanafunzi wengine watatu akidai kuwa, licha ya kuripoti shuleni hapo wazazi wao waliwahamisha na kuwapeleka katika shule za kutwa kwa madai ya kutokuwa na uwezo wa kuchangia chakula.

” Baada ya wazazi wake kumshinikiza aache shule, tulifuatilia na kubaini kuwa mwanafunzi huyo kwa sasa anafanya kazi za ndani katika Mji wa Tunduma,ameleza Kaimu Mkuu wa shule hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, kuwafuatilia wazazi wa mwanafunzi huyo ili wamrudishe aendelee na masomo.

“Mwanafunzi huyu atakapo rudi shule Mkurugenzi hakikisha unampatia mchango huo wa chakula ili aweze kutimiza ndoto zake za kupata elimu, tena nimeambiwa ana uwezo mkubwa darasani,” amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Michael amewaonya wazazi wenye tabia za kuwakatisha masomo wanafunzi huku amewataka kuacha mara moja kwa sababu watakaobainika watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Baadaya ya maelekezo hayo, Mkuu wa Mkoa alikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo mawili ambayo ni nyumba moja ya Mwalimu itakayotumiwa na familia mbili, inayogharimu kiasi cha milioni 100 ambazo ni fedha kutoka Serikali Kuu.