November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mbeya magonjwa yasiyoambukiza chanzo cha vifo ,wananchi fanyeni mazoezi

Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya,Juma Homera amesema kuwa asilimia kubwa ya wananchi wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na msonga wa mawazo.

Kutokana na hali hiyo Homera amehamasisha wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kujenga afya ya mwili ,kuondoa mawazo na kuishi kwa furaha .

Mkuu wa mkoa Mbeya,Juma Homera

Homera amesema hayo Novemba 5, mwaka huu wakati akifungua ,bonanza la Siku ya wanafamilia 2023 kwa Watumishi wa Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) lililofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uhasibu Mbeya (TIA).

“Nawasihi wananchi furaha unaitafuta wewe mwenyewe hayupo ambaye anaweza kukuletea furaha kwenye moyo wako jitahidi kuitafuta furaha ilipo ili uweze kubururudisha moyo, huwezi kuletewa na mtu mwingine na hata akikuletea ataleta kwa muda mfupi bali jitahidi uitafute mimi niendelee kuwasisitiza tufanye mazoezi mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza, “amesema Homera.

Aidha amewataka wananchi mkoani hapa kuendelea kupima afya zao mara kwa mara kwani unaweza ukawa unatembea ukajiona mzima ghafla ukaanguka na kupoteza maisha kwasababu hawana utamaduni huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dkt.Godlove Mbwanji

“Tuna hospitali nzuri kabisa na Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kuleta mashine nzuri za kisasa(MRI) badala ya kwenda jijini Dar es Salaam na Dodoma hivi sasa huduma hizo zinapatikana jijini Mbeya,”amesema Homera.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,Dkt.Godlove Mbwanji amesema wamekuwa wakishirikiana na jamii kufanya nao michezo pamoja na kuhamasisha watu kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Dkt.Mbwanji amesema kuwa moja ya changamoto kubwa ni magonjwa sugu yasiyoambukiza kuongozeka kwa kasi na yamekuwa yakiongeza gharama kubwa kwenye matibabu .

Amesema mkakati wa serikali ni kubadilisha mfumo wa maisha,kupenda kufanya mazoezi na namna ya ulaji wa vyakula pamoja na kupima afya kama mtu ana matatizo na amegundulika mapema uweze kutibiwa kirahisi.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi,Mkurugenzi wa Tiba katika hospitali hiyo Dkt.Uwesu Mchepange amesema kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwakutanisha watumishi wa hospitali wakiwemo wastaafu pamoja na wananchi ili waweze kutambua kazi zinazofanywa na hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya Dkt.Uwesu Mchepange

Amesema kuwa bonanza hilo mpaka Sasa limefanyika mara ya tisa ambapo wamekuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo upimaji wa afya bure ili wananchi waweze kutambua afya zao pamoja na kupata ushauri na shughuli zingine.

Sadock Sanane ni Mtumishi wa Mahakama Kuu amewataka wananchi kujenga mazoea ya kufanya mazoezi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza na kupunguza ulaji usiofaa.

Baadhi ya watumishi wa hospitali Rufaa Kanda ya Mbeya wakiwa kwenye mchezo wa kuvuta kamba