November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mbeya awatoa hofu
wananchi kifo cha JPM

Na Esther Macha,TimesMajira,Online,Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema wapo baadhi ya watu wanaodai kuwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli kitafanya taifa kuyumba kwa kuwa Rais amenyamaza jambo ambalo Mkuu huyo amesema sio kweli.

Chalamila amesema hoja ya kuyumba taifa haitakuwa kweli, kwani wananchi wanaendelea kuliombea taifa ili liweze kusonga mbele na pia kuna hazina kubwa ya viongozi wenye weledi wa kuliongoza taifa bila wasi wasi.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema hayo jana wakati wa ibada maalum ya kumwombea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli pamoja na Rais aliyeingia madarakani, Samia Suluhu Hassan.

Aidha Chalamila alisema katika Kipindi cha majonzi cha kuondokewa na mpendwa wao ni vema kupendana na kutolichafua taifa lao, ndani na nje ya ya nchi.

“Kifo cha mpendwa wetu kisitufanye wananchi kuingiwa na hofu kubwa, kwani kila mtu atapita hiyo njia na kila nafsi itaonja mauti, ni suala la muda tu,”alisema Chalamila.

Mwenyekiti wa Mapadre Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Padre Gaspar Mwangoka aliwataka wazazi na walezi kuenzi mema ya Hayati Magufuli kwa kuhakikisha wanazingatia malezi bora kwa watoto ili waje kuwa viongozi na watumishi shupavu kama alivyokuwa Magufuli.

Amesema Magufuli alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa na kwamba ili kuenzi mema yake yawapasa wazazi na walezi kuwalea watoto katika malezi yanayompendeza Mungu.

Maombi hayo maalum yalifanyika katika uwanja wa Sokoine jijini hapa na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali,chama,pamoja na madhehebu yote ya dini.