Na Esther Macha,Timesmajira Online. Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema kukiwa na ubishani wa kisiasa hawezi kufikia maendeleo wanayotaka, siasa ya kweli ni kuona maendeleo kwani siasa si maneno matupu ni vyema kuhama kwenye maneno matupu na kufanya kazi.
Chalamila ameyasema hayo juzi wakati alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Igawilo unaondelea.
Amesema siasa ya kweli ni kuona majengo yanajengwa, barabara zinatengenezwa kwa kuwa siasa si maneno matupu, kutaka watu kuhama kwenye maneno wafanye kazi kwa bidii ili waweze kusonga mbele.
Hata hivyo amewataka Wakuu wa Idara waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi huo wa hospitali, kujenga uaminifu na kazi ifanyike kwa ufanisi mkubwa.
“Ndugu zangu Wakuu wa Idara leo hii mko mbeya, kesho mnaenda mkoa mwingine leo ni Wakuu wa Mikoa kesho tena raia, hivyo hakikisheni mnasimamia vizuri ujenzi huu hapa ni nyumbani lazima msimamie kikamilifu,” amesema.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa hospitali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dkt. Jonas Lulandala amesema Halmashauri ya Jiji ilipokea sh. bilioni moja kutoka Serikali Kuu Machi mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Igawilo.
Dkt. Lulandala amesema fedha hizo, zitatumika katika ujenzi wa majengo matano ambayo ni jengo la utawala, wodi ya wazazi, jengo la mionzi na jengo la afya ya uzazi na mtoto na jengo la wagonjwa wanawake.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Issa amesema kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji kazi hiyo ya ujenzi, watahakikisha inakamilika mapema ili wananchi waweze kupata huduma.
Naye Diwani wa Kata ya Iganjo, Eliud Mbogela amesema wananchi wa kata hiyo wamekubali mradi uendelee ila wana changamoto ya barabara, ambayo imekatiza ndani ya mradi huo hivyo alimwomba Mkuu wa Mkoa aweze kuwasaidia kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) waweze kuwasaidia.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda