Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amesema kuna haja ya kuwathamini zaidi wataalamu wa afya wanaohudumia watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti),kutokana na mazingira magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika utoaji wa huduma hizo.
Malisa amesema hayo Oktoba 17, 2025, wakati wa ufunguzi wa ukarabati wa wodi ya watoto wachanga (Neonatal Care Unit – NCU) katika Hospitali ya Wazazi Meta, ukarabati uliotekelezwa na Taasisi ya Afya Ifakara (Ifakara Health Institute – IHI) kwa ushirikiano na wadau wa NEST360 Tanzania.
“Kwa wachache tuliobahatika kuona hali ya wodi hii, imenijengea hofu na kunifanya nione thamani ya maisha kwa undani zaidi. Tunapaswa kuwathamini wataalamu hawa kwa moyo mkubwa kwa sababu wanahudumia watoto katika mazingira magumu, wakihitaji upendo na uvumilivu mkubwa,” amesema Malisa.

Ameipongeza Taasisi ya Ifakara na wadau wa NEST360 kwa juhudi za kuboresha miundombinu ya afya, akisisitiza kuwa vifaa vilivyotolewa vitumike ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania, hususan wananchi wa mkoa wa Mbeya.
“Nawashukuru wadau wetu kwa uzalendo wao.Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msingi imara wa miundombinu ya afya, na juhudi hizi za wadau ni mwendelezo wa jitihada hizo. Nikiwa Mkuu wa Mkoa, nitaendelea kushiriki kwa vitendo kila mwaka nitanunua kitanda kimoja kwa ajili ya watoto njiti, chenye thamani ya Sh12 milioni,” amesema Mkuu huyo wa mkoa.
Malisa pia amewataka wadau wengine kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya, hasa kwenye wilaya tano za mkoa wa Mbeya, ili kuhakikisha miundombinu ya hospitali inaboreshwa na kuokoa maisha ya watoto wachanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Ifakara, Dkt. Honorant Masanja, amesema mpango wa NEST360 ulianza kutekelezwa mwaka 2019 hadi 2023 katika awamu ya kwanza, ukiwahusisha hospitali saba, ikiwemo Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
“Kuanzia mwaka 2024 tumeanza awamu ya pili ya mpango huu, ambapo Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Mbeya na Makandana zimeongezwa. Awamu hii inatarajiwa kukamilika mwaka 2028,”amesema Dkt. Masanja.

Amefafanua kuwa mpango huo unalenga kuunga mkono jitihada za serikali kupunguza vifo vya watoto wachanga, ambavyo kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, mtoto mmoja hufariki kila baada ya dakika 10 nchini.
“Asilimia 80 ya vifo hivi vinaweza kuzuilika endapo kutakuwepo na wahudumu wa afya wenye ujuzi wa kutosha, vifaa tiba vya kisasa, na mazingira rafiki ya utoaji huduma,”amesema.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dkt. Godlove Mbwanji, amesema kuwa serikali imefanya kazi kubwa kuboresha sekta ya afya, lakini bado inahitaji ushirikiano wa wadau.
“Tumeona hali halisi kwenye wodi hii ya watoto wachanga inahitaji uwekezaji mkubwa katika vifaa, rasilimali watu na miundombinu. Ni lazima taasisi binafsi na wananchi wajitokeze kusaidia, kwani hawa watoto wadogo ndiyo taifa la kesho,” amsema Dkt.Mbwanji.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi