December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makalla afunga mafunzo ya jeshi la Akiba

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Amos Makalla leo amefunga Mafunzo ya Vijana wa Jeshi la akiba Mgambo Mkoani humo ambapo jumla ya Vijana 659 wamehitimu na wapo tayari kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali ikiwemo Kuimarisha Ulinzi na usalama kwenye Mitaa.

Akifunga Mafunzo hayo Uwanja wa Uhuru, RC Makalla amewaelekeza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwatumia Vizuri Vijana hao kwakuwa wamepata mafunzo na mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu ambapo ameagiza kila ofisi ya Serikali ya Mtaa inakuwa na Mgambo.

Aidha RC Makalla ametoa wito kwa wahitimu hao kushirikiana na Serikali kuongeza Nguvu kwenye udhibiti wa matukio ya uhalifu ikiwemo Vikundi vya Panya Road.

Pamoja na hayo RC Makalla ameelekeza Jeshi la Polis kuhakikisha Kampuni za Ulinzi zinatoa kipaombele wa wahitimu wa mafunzo ya Mgambo na JKT tofauti na Sasa ambapo baadhi wameajiri vijana ambao hawana mafunzo.

Hata hivyo RC Makalla ameelekeza kila Halmashauri kutoa fungu la pesa kwaajili ya kuwezesha mafunzo hayo tofauti na Sasa ambapo Wanafunzi wanajitegemea pesa ya kujikimu.

Katika Mafunzo hayo yaliyohusisha Vijana 659 wakiwemo Wanaume 520 na wanawake 139 wamepata Elimu ya Ukakamavu, Mbinu za kivita, usomaji Ramani, utoaji wa huduma ya kwanza, usalama wa Taifa, Kuzuia na kupambana na Rushwa, utimamu wa mwili,uraia, Kazi za polisi na vita vya msituni.