Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, kupitia idara ya ardhi imetakiwa kuhakikisha inakamilisha majibu ya wananchi ambao wamesikilizwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala Oktoba 17, 2023 wakati wa ziara yake katika halmashauri hiyo ya kusikiliza na kutatua kero.
Ambapo jumla ya wananchi 50 waliwasilisha na kusikilizwa kero zao kupitia ziara hiyo wilayani Ilemela huku akitaka kila mwananchi aliyesikilizwa awe amejibiwa ndani ya siku 14.
“Nataka kupima yale ambayo Mkuu wa Wilaya akiwaelekeza hamtekelezi, itakuwa jambo la ajabu malalamiko haya yasipofanyiwa kazi,tekelezeni maelekezo yote tuliyoyatoa na majibu yapatikane ili tukija siku nyingine tuanze kusikiliza mambo mapya, nataka nikja Ilemela wananchi waseme yale uliyoagiza yamefanyiwa kazi,”amesema Makala.
Pia amewataka watendaji wa idara ya ardhi kubadilika na kutoa huduma inayostahili kwa wananachi kwa kutoa lugha zenye kuleta matumaini kwa wananchi katika kutatua matatizo yao ya ardhi.
“Lugha za kuwahudumia ziwe za staha na zenye matumaini sitaki kusikia malalamiko ya namna mnavyowapokea wananchi wetu,”.
Aidha amesema kuwa amebaini kuwa mambo yaliyochangia katika migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa ni pamoja na upimaji shirikishi kwani inaonesha kampuni zinazopima hazina mawasiliano na ofisi.
Pia hayaratibiwi vizuri lakini viongozi waliopo hawasimamii na kuwajibika ipasavyo katika suala la upimaji shirikishi hivyo ameielekeza halmashauri kuhakikisha inalibeba jukumu hilo.
“Kupima, Kupanga na Kumilikisha (KKK), ni jukumu la Halmashauri hivyo Ilemela hakikisheni mnajiridhisha na kampuni za kupima , uwezo wake, mpango kazi wake,pamoja na kuhakiki kama michoro imezingatia maeneo ya huduma za jamii,” amesisitiza Makala.
Sanjari na hayo amewataka wataalam kuhakiki madeni yote yanayohusiana na fidia kwa watu waliotoa ardhi yao katika taasisi za serikali, wanaodai fidia katika mpango wa kupima,kupanga na kumilikisha (KKK) wanaodai fidia kupisha ujenzi au miundombinu yote yaainishwe.
“Mstahiki Meya uwatake wataalam kuhakiki madeni yote ya ardhi kwani huwezi kutatua tatizo kama hujui ukubwa wa tatizo, ukishajua ukubwa wa tatizo utaweka mipango ya muda mfupi wa kati na mrefu katika kutatua matatizo,”amessma.
Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Renatus Mulunga amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuendesha zoezi hilo la kusikiliza kero za wananchi huku akimuahidi ushirikiano sambamba na kuyafanyia kazi maelekezo huku akiwataka watendaji kutimiza wajibu wao.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba