Na Yusuph Mussa, Timesmajira, Online Korogwe
MKUU wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amemaliza mgogoro wa mipaka kati ya Wilaya ya Korogwe na Lushoto uliodumu kwa zaidi ya miaka 40 kwa kuamua vitongoji vinavyogombewa viende Wilaya ya Korogwe.
Mgogoro huo ulikuwa wa kugombea vitongoji vya Ndulu na Mwisho wa Shamba, ambapo Korogwe wanasema vitongoji hivyo ni moja ya sehemu inayounda Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, wakati Lushoto wanadai vitongoji hivyo ni sehemu ya vitongoji katika Kijiji cha Kiluwai, Kata ya Vuga, Halmashauri ya Bumbuli.
Akizungumza kwenye kikao cha usuluhishi kilichofanyika Ofisi za Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo na kuwashirikisha viongozi na wataalamu wa Wilaya hizo mbili, Kindamba amesema siyo jiografia tu hata huduma za kijamii ikiwet elimu,afya, wananchi hao wanapata Korogwe kwa muda mrefu huku akisema migogoro mingi kwenye Mkoa huo inasababishwa na viongozi kwa maslahi yao binafsi..
Kindamba akitumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuvitaja vifungu vya Sheria kwenye Katiba ya nchi, Biblia na Quran, amesema mwanadamu anaemjua Mungu hawezi kugombea ardhi na kuonya wananchi wasije wakagombea ardhi na kupigana kama ilivyo Somalia, wakati wao ni kitu kimoja.
“Hakuna mtu aliyekuja na ardhi kwenye hii dunia,mwisho wa siku tutarudi kwenye tumbo la ardhi,hivyo, ardhi ni ya Mungu, lakini kwenye sheria za nchi, ardhi yote ipo chini ya Rais, sasa wewe kiongozi au mwananchi, kwanini unagombana na jirani yako sababu ya ardhi!,mnataka tugombane tuwe kama Somalia, maana wale dini moja ya Kiislamu, lakini pia ni jamii moja na bado wanagombana”ameeleza.
Ameeleza kuwa ukiona Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anaingia kwenye migogoro ya ardhi, ujue hasikilizi wataalam na ubinafsi ndiyo chanzo cha kuharibu uhusiano na kuleta migogoro.
“Vitongoji hivi vitabaki Wilaya ya Korogwe na wakurugenzi wa Korogwe na Bumbuli sasa waende wakaweke mipaka kazi nyingine za maendeleo ziendelee” amesema Kindamba.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Diwani mstaafu wa Kata ya Mombo Mohamed Yahaya maarufu ‘Dodoadodoa’ ambaye alikuwa diwani kwa miaka 10 mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, amesema huo mgogoro walishaumaliza,umeibuka awamu ya pili.
Ambapo amesema sababu kubwa ya mgogoro ulikuwa ubinafsi wa baadhi ya viongozi hasa kutaka kuuza viwanja lakini wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Akisoma vifungu vya sheria, na kueleza mipaka ya maeneo hayo, Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa amesema vitongoji hivyo vinastahili kuwepo Wilaya ya Korogwe.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Amir Sheiza, amesema amekubaliana na maamuzi hayo lakini ni sehemu ndogo ya migogoro ya mipaka kati ya Halmashauri ya Bumbuli na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, kwani bado kuna maeneo mengine yana migogoro.
“Sisi Bumbuli na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe bado tuna migogoro kwenye maeneo mengine ikiwemo kitongoji cha Kwebamba kilichopo Kijiji cha Bumba, Kata ya Milingano ambako kuna machimbo ya madini ya vito,kule ni kwetu lakini Korogwe wanasema ni kwao hivyo Mkuu wa Mkoa anatakiwa kuzunguka maeneo yote ili kuweka sawa mipaka,” amesema.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi