Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.
Mkoa wa Katavi umepokea magari manne yenye thamani ya bilioni 1.87, kwa ajili ya Katibu Tawala wa Mkoa huo pamoja na Wakuu wa Wilaya tatu za Mlele,Tanganyika na Mpanda.
Huku Mkoa wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko,akisisitiza kuwa magari hayo yanapaswa kutumia kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Mrindoko akizungumza ofisini kwake Jalai 18, 2024 wakati akikabidhi magari mapya yenye thamani ya Bilioni 1.87 kwa Katibu Tawala Mkoa na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika.
“Magari haya yawe chachu ya kuhakikisha usimamizi wa fedha za miradi unaimarishwa kwa kufikiwa na kukaguliwa,mnapaswa kujiridhisha na matumizi ya fedha yanafuata utaratibu na thamani halisi ya fedha ionekane kwa kila mradi husika iliyoletwa kutatua kero,”.
Katika kuimarisha utawala bora amemwagiza Katibu Tawala Mkoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha shughuli za serikali zinaimarika zaidi hasa utatuzi wa kero za wananchi katika mitaa na vitongoji.
“Kero sio kwenda kusikiliza na kuziandika kwenye madaftari na dairy kisha kuja nazo ofisi na kuziweka mezani. Wakuu wa wilaya tatue matatizo ya wananchi na mfanye maamuzi sahihi yatakayo hakikisha kero na malalamiko ya wananchi yanamalizika na sio kurundika,” amesema Mrindoko na kuongeza kuwa
“Wafahamisheni wananchi kero na malalamiko yao kwamba utatuzi wake ni huu ndicho kifanyike msirundike kero kwani kufanya hivyo ni kutokutekeleza maelekezo ya Mh Rais Dkt Samia”
Katika hatua nyingine amesema kuwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kuduma la wapiga kura ni muhimu wananchi kutumia fursa hiyo muda utakapofika Julai 27, 2024 kujitokeza na kujiandikisha.
“Mwananchi aliye hama eneo lake la awali, kupoteza kitabulisho cha mpiga kura,taarifa zake hazikukaa sawa au katimiza umri wa kupiga kura naombeni mjitokeze kuandikishwa”.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela akitoa taarifa ya ununuzi wa magari hayo amesema kuwa wamepokea magari manne kati yao matatu ni kwa ajili ya Wakuu wa Wilaya ya Tanganyika,Mlele na Mpanda na moja kwa ajili ya Katibu Tawala Mkoa yote yakiwa na thamani ya bilioni 1.87.
Msovela amesema Magari mawili ya Wakuu wa wilaya ya Tanganyika na Mlele kila moja thamani yake ni milioni 193,Gari la Mkuu wa Wilaya ya Mpanda thamani yake ni milioni 224.2 pamoja na gari kwa ajili ya Katibu Tawala Mkoa thamani yake ni milioni 477.4.
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amesema gari ambalo amepata ni kwa maslahi ya wananchi wa Wilaya hiyo yenye ukubwa wa kilomita 16,911 na vitongoji 320 ambapo atatumia kufika kila eneo la kutatua kero za wananchi.
“Jambo kubwa kabisa ninaloliona kama jinsi maagizo ya Mkuu wa Mkoa alivyoelekeza ni kuwafikia wananchi na kutatua kero zao na kuwapa hamasa ya maendeleo na kuwafahamisha ambavyo Rais ameshayafanya katika maeneo yetu ndani ya Wilaya ya Tanganyika,”amesema Buswelu.
More Stories
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo