December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandis Robart Gabriel

RC Geita aanika uongozi wa JPM ulivyoboresha maisha

Na David John, Geita

MKUU wa Mkoa wa Geita, Mhandis Robart Gabriel amesema amelazimika kuacha kugombea ubunge kwao ili aendelee kuwatumikia wananchi wa mkoa huo kwa kutambua kuwa Geita ni kitovu cha madini nchini na ndiyo maana wameweza kujenga masoko tisa ya dhahabu na kati hayo, Soko Kuu la dhahabu liko mkoani Geita.

Amesema na katika kuonesha kuwa Geita ndiyo kitovu cha madini, katika kipindi cha mwaka jana kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa madini nchini na mkoani hapa GGM, iliweza kuuza madini yenye thamani ya sh. tirioni moja na zaidi katika soko la dhahabu.

Hayo ameyasema leo mkoani hapa wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wafanyabishara na wachimbaji wadogo wa madini, huku akiwataka wajasiriamali kuchangamkia fursa mbalimbali kutokana na mkoa huo kuwa ndiyo pekee ambao unazalisha madini ya dhahabu kwa wingi nchini.

“Ndugu zangu wafanyabiashara, nawaomba kwanza kusikiliza kwa makini mafunzo haya ambayo yanatolewa na wadhamini wakuu Benki ya NBC, kwani ni muhimu sana kwa shughuli zenu ambazo mnazifanya kila siku kwenye sekta hii ya madini mkoani hapa, ”alisema.

Ameongeza kuwa wanajivunia kuwa na Rais Jemedari kama, Dkt. John Magufuli, kwani kiongozi huyo ni jasiri na ni mkombozi katika Taifa la Tanzania na alichokifanya Geita, hususan katika sekta ya madini imefika wakati kwa Watanzania kuamka na kuacha kutumikishwa tena na watu kutoka nje ya nchi na anataka wananchi wa Geita, kumiliki migodi yao wenyewe kwa lengo la kufaidi rasimili zao.

Pia amesema anatakiwa kuondoa dhana ya unyonge katika akili zao na kuamini kuwa wao wanaweza na ndiyo maana, Rais Magufuli ameweza kuweka utaratibu mzuri ili kuweza kumiliki mali wenyewe kwa hiyo yeye kama Mkuu wa Mkoa, anampongeza Rais kwa kuweza kunyanyua na kuwajengea uelewa wananchi wa Mkoa wa Geita na kutambua rasilimali zilizopo mkoani hapa.

“Hili eneo ambalo leo mpo lilikuwa jalala lakini sasa linapendeza kama mnavyoona na hapa, tumeshajenga ukumbi wa mikutano na tunaendelea kujenga lakini pia, tumeweza kutenga eneo kwa ajili ya watu wa sekta ya madini na taasisi za kifedha kama vile benki ili waweze kujenga kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wananchi wa Geita,“ amesema.

Amewataka wananchi pamoja na wafanyabiashara, kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kuona mambo mbalimbali yanayofanyika kutokana na uwepo wa madini mkoani hapa.