Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameielekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kuwarasimisha Wafanyabiashara wadogo (Machinga) ili waweze kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.
Senyamule ameeleza hayo Januari 26, 2023 katika viwanja vya Nyerere Square, Jijini Dodoma alipofika kwa ajili ya kuangalia shughuli zinazoendelea katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja hivyo.
Ameeleza kuwa BRELA inatakiwa kuweka jitihada za kuwafikia Wafanyabiashara wadogo bila kusubiri mwaliko wao kwa sababu wengi wao wanaogopa kwamba wanapojirasimisha tozo zinaongezeka katika biashara zao, dhana ambayo siyo ya kweli.
“Mwelekeo wa Serikali ni kuwarasimisha wafanyabiashara wadogo, kwakuwa wanaofanya kazi na Serikali ndiyo wanaonufaika zaidi. Ikumbukwe kuwa asilimia kubwa ya fedha za Serikali zinaelekezwa kwenye manunuzi, hivyo wauzaji wananufaika na fursa hiyo. Kwa hiyo pamoja na gharama za usajili ambazo watalipa lakini faida ni kubwa zaidi”, amesema Senyamule.
Kwa upande wake msimamizi wa Ofisi ya Kanda ya Kati iliyopo Dodoma, Gabriel Girangay amemuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa BRELA itaendelea na jitihada za kuwafikia wajasiriamali na wafanyabiashara wa aina zote kwa kuwahamasisha kuhusu urasimishaji wa biashara zao.
“BRELA inashiriki katika zoezi la utoaji wa elimu kwa umma pamoja na uhamasishaji kupitia maonesho mbalimbali kwa kutoa huduma za papo kwa papo na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza za usajili kwa njia ya mtandao”, ameeleza Girangay.
Ameongeza kuwa BRELA pia hufanya Ukaguzi elimishi katika maeneo ya viwanda na biashara na kuwapa elimu wamiliki jinsi ya kuendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Ametoa wito pia kwa Wafanyabishara kujitokeza kwa wingi pale ambapo BRELA inakuwa ikifanya kliniki za kibiashara katika maeneo yao au kutoa huduma za papo kwa papo katika maonesho mbalimbali ili kupata usaidizi wa haraka.
BRELA itatoa huduma kwa siku kumi (10) mfululizo ambapo huduma hizo zimeanza kutolewa kuanzia tarehe 23 Januari, 2023 na hitimisho litakuwa tarehe 1 Februari, 2023.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba