Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amewataka vijana wa bodaboda kujiepusha na kutotumika katika uhalifu wa mpakani, hususan uvushaji wa bidhaa za magendo.
Akizungumza na kikundi cha bodaboda cha Itumba wilayani Ileje, leo Februari 12, 2025, Chongolo aliwataka waendesha bodaboda kuwa wazalendo na kushirikiana na vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi wa mipaka.
Kikundi hicho cha bodaboda kimefanikiwa kupatiwa mkopo wa pikipiki 10 na pikipiki mbili za matairi matatu (maarufu kama Guta) kupitia mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Katika mkutano huo, mmoja wa madereva, Moses Mkondya, alilalamikia usumbufu kutoka kwa askari polisi wa doria, akidai wamekuwa wakiwakamata kiholela wanapokuwa kwenye shughuli zao za usafirishaji wa abiria abiria katika mji huo wa mpakani wa Itumba.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250212-wa02064064135738193901431-1024x682.jpg)
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa Chongolo alisisitiza kuwa, suala la ulinzi wa nchi si la mzaha, hivyo polisi na vyombo vya usalama vinapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa weledi na bila kusababisha usumbufu usio wa lazima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitumia jukwaa hilo kuwapatia neema vijana hao wa bodaboda ya kuwapeleka lwenye mafunzo ya udereva vijana 26 wanaoendesha bodaboda bila leseni na kuwalipia gharama za leseni zao ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vya kuemdelea kufanya kazi barabarani.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, aliwataka madereva hao wa bodaboda waliokumbwa na manyanyaso kutoka kwa askari kutoa taarifa kwa siri ili hatua zichukuliwe.
Kamanda huyo alitoa namba yake ya simu kwa ajili ya kupokea malalamiko hayo.
Eneo la Itumba, likiwa mpakani kati ya Tanzania na Malawi, limekuwa kitovu cha shughuli za biashara, ikiwemo magendo yanayovushwa kwa kutumia bodaboda.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa Chongolo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, kuhakikisha mkandarasi wa barabara ya Isongole-Isoko anaanza ujenzi mara moja.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250212-wa02053682180775023876869-1024x682.jpg)
Tayari serikali imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Isongole II – Ibungu – Isoko (km 52.419) kwa kiwango cha lami, ambapo tayari waathiriwa wa mradi wapatao 312 wamelipwa jumla ya TZS milioni 850.269 kama fidia ya mali, nyumba na mazao yao.
Barabara hiyo ni muhimu itasaidia kuunganisha mikoa ya Mbeya na Songwe, hivyo kurahisisha usafiri na biashara mipakani, kati ya mpaka wa Kasumulu Wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya, n Isongole Wilayani Ileje na Tunduma, Wilayani Momba, Mkoa wa Songwe ambazo zinapakana na nchi za Malawi na Zambia.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250212-wa02084765212275475317791-1024x682.jpg)
More Stories
Wasira ‘aipiga nyundo ‘No reform no election
Tabora wapongeza uimara wa CCM
CCM yahimiza uadilifu kwa watumishi manispaa Tabora