February 28, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Chalamila kushuhudia mapambano 14 KnockOut ya Mama

Na Mwandishi wetu,Timesmajira online

MASHABIKI wa Ngumi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam leo Februari 28, 2025 wanatarajiwa kuungana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila kushuhudia mapambano makali na burudani ya kipekee kutoka kwa mabondia wa ndani na nje kupitia msimu wa tatu wa KnockOut ya mama.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafia Boxing Promotion Ally Zayumba wakati akizugumza na waandishi katika zoezi la kupima uzito na face-off kwa mabondia hao.

Amesema mapambano hayo makali na ya kipekee yanatarajia kufanyika katika ukumbi wa Magomeni sokoni ambapo
jumla ya mapambano 14 yatafanyika huku yakiusisha mabondia wa ndani na nje ya nchi.

“Nawaomba watanzania na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi siku ya leo kushuhudia mapambano makali na ya kipekee kutoka kwa vijana wetu “amesema Zayumba

Kwa upande wake, Amiri Matumla amehidi kupata ushindi mnono dhidi ya mpinzani wake, Paulo Amavila kutoka Namibia, huku Amavila akijigamba kuwa Matumla bado ni mdogo kwake na hana nafasi ya kushinda.

Katika hatua nyingine Kampuni ya Mafia Boxing Promotion pia imetoa mitungi ya gesi kwa wanawake wajasiriamali ili kuwawezesha kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamasisha matumizi ya gesi kama chanzo safi cha nishati.

“Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeamua kutoa mitungi ya gesi Kwa mama lishe hawa katika kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia kama gesi na umeme badala ya kuni na mkaa” amesema Zayumba