November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chalamila, Yonazi washiriki mbioo za IFM

Na  Mwandishi Wetu Dar Es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameshiriki IFM Alumn Marathon ambayo imeandaliwa na Watumishi na Wanafunzi waliosoma katika chuo cha Usimamizi wa (IFM) ambao kwa sasa wanafanya kazi maeneo mbalimbali hapa nchini.

Akiongea Nov 19,2023 mkoani Dar Es Salaam mara baada ya kukimbia umbali wa kilometa 5 Chalamila amekipongeza chuo hicho kwa kubuni matembezi hayo ambayo mapato yanayopatikana yanatumika katika maendeleo ya Chuo. 

“Jambo linalofanywa na IFM ni la Kizalendo nitoe rai kwa vyuo vingine kuiga mfano huo wa kibunifu ambao una masilahi mapana sio tu kwa chuo bali hata Taifa kwa ujumla” amesema Chalamila

Aidha amewataka kufanya maboresho katika matembezi hayo kwa kushirikisha makundi mengi zaidi kwa mfano kundi la jogging ili kuweza kusambaza ujumbe ufike mbali zaidi, vilevile ametoa Salamu za Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo amesema Rais anawasalimu na anafurahishwa na kitendo hiki cha kutambua umuhimu wa mazoezi katika Afya ya Binadamu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni mwenyekiti wa umoja huo naye ameshiriki mbio hizo kwa umbali wa kilomita 5.

Dkt. Yonazi amesema kuwa marathon hiyo imehusisha watu ambao walisoma IFM, na marafiki ili kuleta umoja wa wana IFM na kuongezea kuwa mbio hizo huchangia maendeleo ya Chuo na Taifa, pia amewashukuru wadhamini wote waliojitoa kwa hali na mali kuwezesha kufanyika kwa mbio hizo.

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho Dkt. Mnzava amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuungana nao katika mbio hizo ambapo amesema ni tukio la kihistoria na ni mara ya kwanza toka chuo kianze mwaka 1972, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuendeleza mbio hizo, kwa kuhamasisha makundi mbalimbali kushiriki kwa kuwa mazoezi ni Afya kama kauli mbiu inavyosema ” Badili Mwenendo Wako wa Maisha kwa Afya Bora”