Na Penina Malundo,Timesmajira
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila amesema maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu sabasaba ni kielelezo cha diplomasia na uhusiano wa kimataifa uliopo kati ya Tanzania na mataifa mengine.
Amesema maonesho hayo kwa mwaka huu yatakuwa ya tofauti na miaka mingine yote ya nyuma kwani hadi sasa tayari washiriki wa ndani na nje zaidi ya 3000 wamethibitisha kushiriki.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam,Chalamila wakati alipofanya ziara ya kukagua mabanda na kufungua semina ya kuwajengea uwezo washiriki wa maonesho hayo ya DITF.

Amesema Uhusiano huo wa kimataifa umejikita katika sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, Toleo la mwaka 2024 iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, unataka kuonesha kwamba Tanzania utakuwa na uhusiano wa kimataifa lakini pia itafanya mambo gani katika mahusiano hayo.

Amesema miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na maonesho ya SABASABA ambayo ni fursa ya wafanyabiashara kujitangaza na kutangaza biashara zao.
“Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam mnatakiwa kuacha kusifia Maonesho ya 49 Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu sabasaba badala yake tumieni kama sehemu ya washiriki watakaotangaza na kuuza biashara zao katika viwanja vya maonesho hayo.
“Wananchi wa Dar es Salaam wasipotumia fursa ya uwepo wa maonesho hayo basi watabaki kuwa watu wanaowakaribisha wengine kutoka mikoa mbalimbali kuja kufanya biashara na wao kubaki nyuma.

“Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tusibaki kusifu maonesho ya sabasaba huku tukiwa tumelala kitandani na kuwa sio sehemu ya maonesho haya, niwaombe vijana, wanawake, kinababa tutumie fahari ya maonesho haya kuwa sehemu ya wale wataofanya biashara,”amesema
Aidha Chalamila amesema maonesho hayo hayafanyika Dar es Salaam kwa bahati mbaya bali ni kwa sababu ni mahali ambapo watu wengi wanaweza kufika na kufanya biashara zao hivyo amewataka watanzania kukaribia katika viwanja hivyo kuonesha bidhaa zao.

Akiwa katika viwanja hivyo vya SABASABA RC Chalamila alipata wasaa wa kusikia taarifa fupi ya maandalizi ya maonesho hayo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo,Latifa Khamis na kisha kutembelea mabanda mbalimbali yaliyoko ndani ya viunga vya SABASABA.
Khamis amesema maonesho ya mwaka huu ni tofauti na miaka mingine kwa kuwa yameandaliwa kidijitali zaidi kwa kuwa hata wakati wa kuomba ushiriki ilikuwa Online, ukataji Ticketi.

Amesema pia mwaka huu mitandao mbalimbali ya simu itatumika kukata tickets vilevile kutakuwa na usafiri wa kuzunguka ndani wa kisasa kabisa ambao utatolewa na shirika la Posta, pia kutakuwa na kijiji cha burudani na kijiji cha michezo hivyo wananchi watarajie mambo mengi mazuri.
RC Chalamila ameridhia ombi la usafiri wa mabasi ya Mwendokasi kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri kwa kipindi chote cha maonesho ya SABASABA 2025.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi