Na Judith Ferdinand,TimesMajira online,Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Albert Chalamila ametoa rai kwa watu wanaotumia vibaya misamaha inayotolewa na Serikali ikiwemo ya huduma za afya na kodi kuacha tabia hiyo.
Ametoa rai hiyo wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkoa mkoani hapa.
Chalamila amesema,kumekuwapo watu wanatumia vibaya misahama inayotolewa na Serikali na kutolea mfano huduma ya afya ambapo kuanzia watoto wa miaka mitano na wazee wa miaka 60 wanapaswa kupata huduma za matibabu bure, lakini wapo wazee wenye uwezo wanavizia huduma hizo.
“Lakini unakuta mzee ana uwezo amekuja na Prado hospitalini na kuliegesha nje, lakini bado anakuja kuvizia kupata huduma ya Panadol za bure, hiyo si sawa”amesema Chalamila.
Pia amesema,baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanatumia fursa ya vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo (machinga) kufunga maduka na kuwapa bidhaa zao machinga wawauzie kwa sababu wanatumia vitambulisho vya 20,000, kwa mwaka.
Amesema wafanyabiashara hao wanatumia fursa hiyo ya misamaha ya serikali vibaya kwa kuwapa bidhaa wafanyabiashara wadogo wadogo na hivyo kukwepa kulipa kodi.
Chalamila,amesema baadhi ya wachimbaji wadogo ambao kila siku wanajiita hivyo na wanafurahia,hawataki kuitwa wachimbaji wakubwa wala wa kati kwa vile wanajua ukiwa mchimbaji mdogo kuna baadhi ya kodi zimeondolewa.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza amesema serikali imetoa fursa hizo kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kuwajengea tabia ya kulipa kodi ndogo ndogo na matarajio ya serikali ni kuona wanakuwa wafanyabiashara wakubwa .
“Vijana hao leo tunawafundisha kulipa kodi kidogo kidogo lengo wasije kuwavizia huko juu na kuwatoza kodi wakishakuwa wakubwa kibiashara watakuwa wakweepa kodi.Kuna gharama kubwa za uendeshaji wa huduma za afya, miradi mbalimbli ya maendeleo ya nchi, hivyo watu wasiitumie vibaya misamaha ya serikali,”amesistiza Chalamila.
Aidha amewataka machinga kujipanga vizuri na kufanya baishara kwenye maeneo rasmi na kuchana na mtindo wa kupanga bidhaa na kufanya biashara kwenye maeneo ya barabara na wazi ambayo si ya kibiashara ilii kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake wa kuhudumia jamii.
Naye Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Uhuru, Derick Nyasebwa, amesema wananchi walio wengi wamejikita kuchangia arusi kuliko kujiunga na Bima ya Afya ili kuwasaidia na kuweza kugharamia huduma hizo.
“Watu wengi wanatumia misamaha ya huduma za afya vibaya kwa kuchangia arusi na sherehe mbalimbali, wanashindwa kulipia ama kukata bima ya afya,wito wangu wakate bima ili misamaha hiyo itumike kwa watu wasio na uwezo,”amesema Nyasebwa.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara Mwakilishi wa Mkurugenzi kutoka Birchand Groupb Mohamed Ibrahim amesema wanaimani watashirikiana vyema na Chalamila katika kuleta maendeleo ya Mkoa na nchi
“Tunashukuru kwa ushirikiano tulioupata kutoka kwa serikali ya Mkoa ya aliyekuwa Mkuu wetu wa Mkoa John Mongella, tunaimani na Chalamila atafanya vyema kama alivyotuahidi,”amesema Ibrahim
Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Maji Batul Seif,amesema watatoa ushirikiano hususani katika kutekeleza adhima ya serikali ya kuleta maendeleo ya Mkoa hasa kwenye suala la zima la usimamizi wa rasilimali za maji hususani tekelezaji wa sheria yetu ya usimamizi wa rasilimali kwa kuzingatia sera ya maji ya Taifa ya mwaka 2002.
More Stories
Wizara ya Nishati yawasilisha utekelezaji wa bajeti 2024/2025 kwa Kamati ya kudumu ya bunge Nishati na Madini
Watanzania milioni 13.5 kusambaziwa umeme ifikapo 2030 kutoka milioni 5.2 ya sasa
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji