December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Chalamila amshukuru Samia kwa uwekezaji sekta ya mifugo

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amekabidhi pikipiki 24 zenye thamani ya milioni 72 kama vitendea kazi kwa sekta ya mifugo katika mkoa huo na amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza sekta ya mifugo .

Akizungumza na wataalam waliopokea pikipiki hizo kutoka wilaya zote za mkoa huo, Chalamila alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa jitihada yake kubwa za kuboresha sekta mbalimbali hapa, nchini ikiwemo sekta ya mifugo ambapo kupitia wizara ya mifugo na uvuvi ametoa pikipiki hizo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha, RC Chalamila aliwataka wataalam hao kutumia pikipiki hizo vizuri,kwenda kuelimisha na kuhamasisha jamii ufugaji wa kisasa na wenye tija ambao utawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Vilevile ametoa taadhari ya matumizi mabaya ya vyombo hivyo kwa kuwa ni vyombo vya moto ni vema vitumike kwa uangalifu mkubwa.

Naye Katibu Tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Mkoa, Dkt. Elizabeth Mshote, alisema sekta ya mifugo katika wilaya zote za Mkoa wamepatiwa pikipiki 24 kwa mgawanyo tofauti.

Akitaja mgawanyo, alisema Halmashauri ya Jiji imepata pikipiki tano, Kinondoni nne, Temeke tano, Ubungo tano, na Kigamboni tano. Alisema watumishi ambao wamepata pikipiki na wana leseni ya kuendesha pikipiki ni 14 kati ya 24

Alisema Mkoa wa Dar es Salaam una wafugaji wengi hasa ufugaji wa kisasa, hivyo kupatikana kwa vitendea kazi hivyo kunakwenda kuinua sekta hiyo muhimu kwa masilahi mapana ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.