Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ameagiza kuundwa kwa tume maalum ya wataalamu kuchunguza kwa kina namna mabaraza ya kata yanavyoshughulikia migogoro ya ardhi, akisema hatua hiyo inalenga kuongeza uwajibikaji na kupunguza malalamiko ya wananchi.
Akizungumza katika kikao cha utatuzi wa migogoro hiyo, RC amesema tume hiyo itaundwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali na itafanya kazi kwa kipindi cha miezi miwili kwa majaribio (pilot) kabla ya uamuzi wa utekelezaji wa kudumu. Alifafanua kuwa tathmini itakayofanyika itasaidia kubaini changamoto na kutoa mapendekezo ya maboresho kwa manufaa ya wananchi na Serikali.
Aidha, amewaonya viongozi wa mitaa na kata dhidi ya tabia ya kusaini nyaraka na baadaye kujitenga zinapojitokeza changamoto. Amesisitiza kuwa kila kiongozi anawajibika kisheria kwa maamuzi anayoyafanya, huku akibainisha kuwa Serikali Kuu hutegemea taarifa za Serikali za Mitaa katika kupanga na kutekeleza bajeti.

RC huyo pia ameagiza kuwasilishwa kwa wasifu wa watendaji wa mitaa na kata ili kuhakikisha kila mmoja anapangiwa majukumu kulingana na sifa na uwezo wake, akisema kuna dalili za mapungufu katika baadhi ya maeneo zinazohitaji marekebisho ya haraka.
Kuhusu mamlaka ya mabaraza ya kata, ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria, mabaraza hayo yana jukumu la kushauri na si kuhukumu kama mahakama. Hivyo, ameagiza wajumbe wake kupewa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria za ardhi ili kuepuka migogoro na kutoa ushauri sahihi kwa wananchi.

Ameongeza kuwa migogoro mingi ya ardhi huchochewa na tamaa ya mali, akiwataka viongozi na wananchi kuzingatia haki, uadilifu na kufuata taratibu za kisheria ili kuimarisha amani na imani kwa Serikali.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina