Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Mtwara
MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ametoa wito kwa Ushirika kuangalia namna bora ya kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kwa Vyama vya Ushirika kuwa na maeneo ya mashamba yao ya uzalishaji zao hilo.
Mkuu wa Mkoa Byakawa ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama Kikuu cha Masasi, Mtwara Cooperative Union (MAMCU), katika Chuo cha Ualimu Mtwara.
Amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kuwa na maono makubwa yenye uendelevu wa zao la korosho utakaosaidia kilimo hicho kuwa endelevu na kuongeza uzalishaji wa Korosho.
“Ili tuwe na zao endelevu lenye uhakika na usalama wa uzalishaji lazima ushirika uwe na mashamba yao ya Korosho ardhi haiongezeki, hivyo tuangalie namna bora ya kutumia mapori na ardhi isiyotumika kwa kufuata taratibu zilizopo kuongeza mashamba ya Korosho,” amesema.
Mkuu wa Mkoa huyo ameeleza kuwa ni wakati sasa kwa wakulima wa korosho kuwajibika katika kuhakikisha kuwa uzalishaji wa zao hili unaongezeka kwa kufuata kanuni za kilimo bora kama vile matumizi ya mbegu bora, umbali wa mikorosho shambani, kujua tabia na utunzaji sahihi wa mikorosho.
“Wakulima wengi mmerithi mikorosho ya miaka mingi isiyozaa na pengine hamjui hata alipanda nani, mnaachia mapori kuchanganyika na mikorosho, hamtumii mbinu za kisasa za Kilimo, niwaombe sana tubadilike,” amesema RC Byakanwa.
Ameongeza kuwa wakulima wa korosho wanaweza kuleta mapinduzi chanya ya kilimo cha Korosho kwa wakulima kuamua kuchukua hatua stahiki za kuwajibika na kilimo chao wenyewe kabla ya kuangalia changamoto nyingine.
Moja ya ajenda kuu za Mkutano huo ni pamoja na uchaguzi wa viongozi wa wajumbe wa Bodi wa pamoja na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU.
Hivyo, RC Byakanwa amewataka wajumbe wa Mkutano huo kuchagua viongozi waadilifu, wanaoweza kusimamia Ushirika kwa kuwa na elimu, viongozi wenye maono na mikakati ya kuendeleza Chama na Ushirika kusonga mbele.
“Tumieni haki na demokrasia yenu vizuri kwa kuchagua viongozi wenye sifa, viongozi wenye maadili na uadilifu mkubwa msichague viongozi ambao baada ya siku chache watatuingiza kwenye migogoro,” amesisitiza RC Byakanwa.
RC Byakanwa amepongeza miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU ikiwa ni pamoja na maghala ya yanayojengwa ikiwemo ghala la Ndwika wilayani Nanyumbu Halmashauri ya Masasi, ghala la Ntimbwilimbwi Wilaya ya Nanyamba Halmashauri ya Mtwara.
Akisoma taarifa ya mwenyekiti anayemaliza muda wake wa uongozi wa MAMCU, Joseph Kidando ameeleza Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Ltd kinahudumia wakulima kutoka maeneo ya Nanyumbu, Masasi Mji, Masasi Vijijini, Mtwara Mji, Mtwara Vijijini pamoja na Halmashauri ya Nanyamba chenye wanachama Vyama vya Ushirika vya msingi vipatavyo 164 mkoani Mtwara.
Amebainisha kuwa shughuli kuu za chama hicho ni pamoja na usimamizi, uhifadhi na utafutaji wa masoko ya mazao ya wakulima mkoani Mtwara.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi