Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian ameunda Kamati ya watu 6 ili kuchunguza tukio la Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya Sikonge kumbaka mama mjamzito aliyekuja kupata matibabu.
RC amechukua hatua hiyo baada ya kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na Mtumishi huyo wa umma na mbaya zaidi ikibainishwa kuwa alikuwa amelewa.
Alisema licha ya kuwa mtuhumiwa amefunguliwa kesi, ameamua kuunda kamati ili kuchunguza undani wa tukio na kujiridhisha kama kuna uzembe au matukio mengine yanayofanana na hayo.
Alibainisha kuwa mtumishi huyo ana mwaka mzima tangu aajiriwe na serikali kutumikia wananchi, kama alikuwa na tabia kama hiyo alipaswa kubainika mapema na kuonywa, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa na hakuna aliyembaini.
Akinukuu taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa, RC Batilda alisema mtuhumiwa alikiri wazi kuwa alikuwa na msongo wa mawazo ndio maana akamwingilia mama huyo.
‘Hapa kuna kitu, ndio maana nimeunda kamati hii ili tuchunguze undani wa tukio hili na kuchukua hatua stahiki itakapobidi, tunataka akinamama na wananchi wote kwa ujumla waendelee kupata huduma za afya katika hospitali hiyo’, alibainisha.
RC alifafanua kuwa vitendo vya ukiukaji maadili ya utumishi wa umma vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara ikiwemo cha hivi karibuni cha kifo cha mapacha wachanga kilichotokea wilayani Kaliua, Kituo cha Afya Kaliua cha kunyofolewa jicho na kuchunwa ngozi ya uso kichanga.
Aliongeza kuwa Kamati hii itasaidia kuibua madudu mengine wanayofanyiwa wagonjwa wanapoenda kupata huduma za afya ambayo ni kinyume na maadili hivyo kukomesha tabia za namna hiyo.
Aidha kutokana na tukio hilo, aliagiza Wakuu wa wilaya zote Mkoani hapa kukutana na timu za afya za wilaya zao ili kuwakumbusha wajibu wao na kuwaeleza nini serikali inachotaka kutoka kwao.
Alibainisha kuwa baada ya kukutana na timu za afya aliwataka kukutana na walimu na Maafisa Elimu wote wa kuwapa mwelekeo wa nini Mkoa unahitaji kutoka kwao na si vinginevyo.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM