November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC atoa siku 7 familia zinazoishi bonde Wembere kuondoka

Na Tiganya Vincent,TimesMajira online,Tabora

FAMILIA kumi za wafugaji na wakulima ambazo bado zilikuwa zimebaki katika eneo la Bonde la Wembere lilipo wilayani Igunga licha ya wenzao kutii maagizo ya Serikali zimepewa siku 7 kuondoka hiari kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati alipofanya ziara katika eneo la Bonde la Wembere kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa agizo la kuwataka watu waliokuwa ndani ya bonde hilo kuondoka kwa hiari.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt.Philemon Sengati (mwenye suti ya bluu) akitoa maagizo jana kwa kaya 10 ambazo bado zinaendelea kukaidi kuondoka katika bonde la Wembere wilayani Igunga ndani ya siku saba ziwe zimeondoka.

Amesema hadi hivi sasa zaidi ya familia 200 zimeondoa kwa hiari katika eneo hilo na kwenda katika eneo maalumu ambalo wapengangiwa na Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na Wilaya lakini hizo familia 10 zimeendelea kubaki licha elimu waliyopatiwa katika mkutano wa hadhara.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema katika mkutano na watu hao ulifanyika katika kijiji cha Makomero mapema mwezi uliopita walikubaliana kaya 13 kati ya 200 ambazo zilikuwa bado ndani bonde hilo ziondoke na ziende eneo walilopangiwa,lakini ni kaya tatu ndio zilitekeleza agizo hilo na kaya 10 zimendelea kubaki.

Amesema kusuasua kwa familia hizo kuondoka kunasababishwa na baadhi yao kuwapotosha kuwa wasiondoke .

Mkuu wa Mkoa wa Tabora ,Dkt. Philemon Sengati (mwenye suti ya bluu) akiangia jana mmoja ya nyumba ya wanakaya 10 ambao bado wanaendelea kukaidi agizo la kuwataka kuondoka katika bonde la Wembere wilayani Igunga

Kufuatia hali hiyo,Dkt.Sengati alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo kwa kushirikiana na Polisi wa Igunga kumtafuta kinara wa mgomo huo ambaye ni kiongozi wa kundi la wakulima Kilimanjalo Masandu Masaganya na wenzake wawili ambao wamekuwa wakiwahamasisha wenzao kutoondoka ili kujua nani yuko nyuma yao.

“Hizi kaya 10 zilizobaki ndani za siku 7 ziondoke ili Serikali iweze kutekeleza majukumu yake katika eneo hili …ndani za siku saba sitarajii kuzikuta kaya hizi zikiwa bado ndani yake, amesisitiza.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa hatarajii kuona wanasiasa wanatumia siasa katika eneo hilo ambalo lina maslahi mapana kwa maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa Tanzania sio kisiwa imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ya kutunza na kuhifadhi maeneo oevu.

Amesema ni kinyume cha sheria kaya hizo kuendelea kuwemo humo, kwa kuwa eneo hilo ni mali ya Serikali na linayo maslahi mapana ya nchi ikiwemo utafiti wa gesi na mafuta unaondelea na eneo hilo ni chujio la maji kuelekea Ziwa Eyasi.

Dkt.Sengati ametaja maslahi mengine yanayopatikana humo ni pamoja na uwepo wa aina ya Flamingo ambao wanapatikana maeneo machache duniani na bonde hilo ni njia ya wanyamapori kuelekea Pori la akiba la Rungwa.

Kufuatia Mkuu huyo wa Mkoa amesema ofisi yake itafanya majadiliano na Ofisi ya Makamu Rais Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Nishati , Wizara ya Maji na Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makazi ili waweze kuanisha eneo ambalo lina maslahi mapana ya nchi na litakalobaki wapewe wananchi kwa utaratibu mzuri.

Amesema kaya zilizobaki katika eneo hilo zimejimilikisha maeneo makubwa ambayo ni mali ya Serikali na kuyatumia kwa maslahi binafsi ya kuwakodisha wafugaji kutoka maeneo mbalimbali kulisha mifugo yao na kuendelea kusababisha uharibifu katika bonde hilo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema wataendelea kuhakikisha maeneo yote ya hifadhi yanalindwa na kuzuia wavamizi kuingia kwa ajili ya kuendesha uharibifu ndani yake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga (OCD), Ally Mkalipa amesema Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Igunga imekwenda katika eneo hilo ili kutathimini kaya zilizomo ndani yake na kukaa nao kikao wakakubali na kuonyeshwa eneo watakalohamia ambao walilipenda na kaya nyingi zilihamia na kuondoka katika bonde hilo , lakini kuna kaya ambazo zimekataa kuhamia katika sehemu walizopangiwa.

Amesema kitendo cha familia 10 kuendeleaa kubaki ni ukaidi na kukiuka makubaliano na hivyo watachukua hatua kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Nchi.

Mkalipa amesema familia hizo ni wakaidi kwa kuwa watumia mbinu za wanaume kujificha nyakati za mchana na kuacha watoto na wanawake na ikifika usiku ndipo wanarudi na baadhi yao wanadiriki hata kuwahamasisha wenzao wasiondoke kwenda walipopangiwa na Serikali ya Kijiji kwa kushirikiana na Wilaya.