November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Tabora Dkt. Philemon Sengati,

RC aagiza kukamatwa Mwenyekiti wa kijiji Mdaki

Na Tiganya Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Tabora Dkt. Philemon Sengati, ameagiza kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mdaki wilayani Uyui, Charles Wambo kwa tuhuma za kuchangisha michango kinyume cha taratibu na kuwapatia stakabadhi zinaonesha fedha walizotoa.

Alitoa agizo hilo mjini Tabora baada ya Mwenyekiti huyo kutuhumiwa kuwa amekuwa akipita kwa kila familia na kuchangisha kiasi cha sh. 15,000 kwa madai kuwa anazipeleka polisi ili wasiwe wanakwenda usiku kuendesha misako katika kijiji chao.

Dkt. Sengati amesema mhusika ni lazima akamatwe na kufikishwa katika
vyombo vya sheria ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amewataka wananchi kuishi kwa kuzingatia sheria zinazoongoza nchi na
kutopenda kutoa fedha kwa nia ya kutaka kuficha maovu. Dkt. Sengati
amesema serikali haina utaratibu kukusanya fedha kwa lengo kutaka
kuzuia misako ya kutafuta waharifu.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora amekabidhi kiasi
cha shilingi milioni 185.3 ziliokolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tabora kutoka kwa wabadhirifu.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Mussa Chaulo amesema kati ya fedha hizo shilingi milioni 103.4 zilirejeshwa kwa wakulima waliouza tumbaku kwenye chama cha Ushirika cha Imalamakoye AMCOS ya Urambo.

Amesema fedha nyingine ni kiasi cha sh. milioni 16.5 ziliokolewa baada
ya Nyota ya Muungano AMCOS kulipa kama gharama za ujenzi wa ghala
lakini halikujengwa na mkandarasi.

Chaulo amesema kiasi 38.1 ziliokolewa baada ya MIBONO AMCOS ya Sikonge kukatwa na Igalula AMCOS kimakosa kupitia kuuza tumbaku.

Ameongeza kuwa sh. milioni 25.4 zimeokolewa na kurejeshwa na Chama
Kikuu cha Ushirika WETCU baada ya kukatwa kimakosa kama gharama za
kusambaza mifuko 660 ya mbolea ya NPK.