Na Philemon Muhanuzi, Times Majira Online
RATIBA ya msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara imeshatolewa na shirikisho la soka nchini TFF. Na imeshawafikia walengwa wote. Wale wanaosafiri kwenda kuanza msimu kwa mechi za ugenini wameshasafiri na kufika.
Wanaoanzia nyumbani wanaisubiri timu kutoka ugenini. Kila uongozi wa kila timu unajipanga kwa kuangalia masuala muhimu kama vile mpangilio mzima wa ratiba kulingana na pesa ya mgao kutoka TFF na vyanzo vinginevyo.
Huu ni msimu wa ligi kuu utakaokumbukwa katika historia kwani ni wa kwanza tangu ugonjwa wa Corona uvuruge ratiba za kila shughuli ya kijamii ya dunia hii.
Kufika mwezi wa tisa kwa kawaida msimu unakuwa umeshaanza kusogea huku mechi kadhaa zikiwa zimeshachezwa. Lakini Corona imeharibu kila kitu kuhusiana na mazoea ya miaka yote.
Mabadiliko ya ratiba kwa msimu huu yamekumbana na kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea. Haitakuwa ajabu kusikia ratiba ya ligi kuu imeanza kupanguliwa.
Sababu itakuwa ni kupisha mikutano ya kampeni. Mara nyingi kampeni zinafanyika katika eneo kubwa ambapo watu wanaweza kusimama na baadhi wakawa wameketi wakiwasikiliza wagombea wakinadi sera zao.
Na viwanja vilivyojengwa na chama tawala miaka takriban arobaini iliyopita hutumiwa kwa ajili ya kampeni hizi za kisiasa.
TFF wakiwa ndio wenye jukumu la kuendesha ligi kuu wanaweza kujikuta wakilazimika kufanya maamuzi yasiyokuwa yamepangwa kufanyika ili kwenda sambamba na ratiba za vyama vya siasa.
Hapo ni lazima vilabu na vyenyewe viwe na wepesi wa kujipanga katika kwenda sambamba na hayo mabadiliko ya ratiba yasiyotegemewa kwao.
Ndipo zinapoibuka gharama mpya kabisa za timu kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Pesa itakayotumika kwa ajili ya kusafirisha timu inakuwa haipo katika lile fungu linalotoka TFF kwa kila klabu inayoshiriki ligi kuu.
Huo ndio mtihani wenye kutarajiwa kuwakuta viongozi wa vilabu vya ligi na wale wa TFF. Wenye viwanja kwa maana ya wale waliovijenga miaka iliyopita mwaka huu wanavitumia.
Ni vigumu kwa vyama vya siasa kukubali kufanyia kampeni katika maeneo ya wazi ya nje ya miji, mahali ambapo pengine umeme haupo.
Watajikuta wanatumia viwanja vyenye miundo mbinu ya umeme, vyoo, na masuala mengine yenye urafiki na uwepo wa maelfu ya watu kwa wakati mmoja.
Ni msimu wa ligi utakaoanza katika hali isiyo rafiki kwa ligi kuu na mambo yatarudi katika hali ya kawaida baada ya uchaguzi kuwa umeshamalizika.
Na uzoefu wa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ni kwamba viwanja vinachakaa sana baada ya shughuli za kisiasa kuwa zimemalizika.
Nyasi zinapoteza kabisa ubora wake, michoro ya pembeni na katikati ya uwanja inakuwa imefifia. Panakuwa pakihitajika umwagiliaji wa maji wa siku kadhaa ili ubora wa awali uweze kurudi.
Hata kabla ya matumizi ya kisiasa, nyasi za viwanja vingi huwa na kiwango duni sembuse baada ya wafuasi wa vyama kuwa wamerukaruka wakicheza muziki wa kampeni!.
Wa kuvisemea viwanja hivi ni wote wanaovitumia wakati wa ligi kuu, kwa maana ya TFF na viongozi wa vilabu.
Waandishi wa habari za michezo ni watu wenye jukumu la kuwakumbusha wanasiasa kwamba viwanja haviwezi kujitetea ili viwe na ubora wa kimataifa. Kampeni zikiwa zimeshamalizika na kura zikawa zimeshapatikana kinachofuata ni utekelezaji wa ahadi.
Ukarabati wa viwanja vinavyotumika katika kuwajulisha wapiga kura juu ya nini kinachokwenda kufanyika ili maisha yao yawe bora zaidi, ni jambo ambalo pengine linakuwa likisahaulika mara kwa mara.
Nawapa pole ya awali kabisa viongozi wa TFF, viongozi wa vilabu na wachezaji kutokana na ratiba za baadhi ya mechi kuingiliana na ratiba za mikutano ya kampeni.
Ikiwa hata mchezo wenyewe wa soka umeweza kuanza kuchezwa tena kwa maamuzi magumu ya Mheshimiwa Rais John Magufuli kipindi hiki cha Corona, hizo mechi za ligi kuhamishwa viwanja vya kuchezewa ni jambo ambalo halipaswi kuwapa unyonge wahusika.
Kunung’unika huwa hakuleti mabadiliko wakati baadhi ya mitihani inapomkumba mwanadamu. Corona ilipoingia nchini ikabidi ligi kuu isogezwe mbele, baada ya kumalizika na msimu mpya kuanza kipindi cha kampeni na chenyewe kimeanza.
Mwaka 2020 una namba zenye kugawanyika na machoni zinaonekana kuwa nzuri lakini cha kushangaza umekuwa hauna bahati kama namba zenyewe zilivyo.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM