November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RATCO atetea nafasi yake ya NEC

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Tanga

MJUMBE wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokea Mkoa wa Tanga Mohamed Salim ‘RATCO’ ameweza kutetea nafasi yake baada ya kuchaguliwa kwa kura 778.

Kwenye uchaguzi huo uliofanyika Novemba 22, 2022 jijini Tanga, ulikwenda sambamba na nafasi mbalimbali za viongozi ikiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga.

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, alisema Salim alipata kura 778, huku mshindani wake wa karibu Hassan Bomboko akipata kura 563, huku Omar Sempoli akipata kura 47.

Rajab Abdallah alitangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Tanga baada ya kuwashinda wenzake wawili.

Abdallah alipata kura 1,340, huku Mathias Mkangwa akipata kura 29 na Derick Kazoba kura tisa.

Katika uchaguzi huo, wanachama wawili kila wilaya, walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tanga, ambapo Hussein Ngaga na Halima Mussa walichaguliwa kushika nafasi hiyo kutoka Wilaya ya Korogwe Vijijini (kichama)Lushoto ni Mwanahamis Juma na Faraha Mvumo, Kilindi ni Twaha Mbwego na Abdallah Killo, Mkinga wapo Salum Badi na Mohamed Mwanyiro, Wilaya ya Korogwe Mjini (kichama) ni Mathew Mganga na Omar Zubeir.

Wilaya ya Muheza ni Shifaa Chiwaga na Hamis Ngoda, Pangani wapo Swahibu Manyoka na Omar Janja, Handeni ni Feruzi Banno na Dkt. Hamza Kabelwa, na Tanga ni Habiba Namalecha na Nassoro Makau.

Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Selemani Mzee (kushoto) akimtambulisha mgombea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Mohamed Salim ‘RATCO’ (katikati), kabla hajaanza kujieleza kuomba tena nafasi hiyo. RATCO alishinda uchaguzi huo kwa kura 778. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga aliyemaliza muda wake Dkt. Henry Shekifu akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Mkoa wa Tanga. Ni kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 22, 2022 jijini Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Wagombea wa nafasi mbalimbali wa CCM ngazi ya Mkoa wa Tanga. Ni kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 22, 2022 jijini Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi Mkoa wa Tanga. Ni kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 22, 2022 jijini Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).